Tuesday, April 5, 2022

AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)

http://bit.ly/3JGDJ4d

MWL. JAMES F. MZAVER

Minister Truth

0762759621

jamesmzava@gmail.com




            AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)



Ukuaji hauwezekani bila chakula kizuri na bora. Kubadilika kwa muumini kunawezekana tu wakati watu wanalishwa neno kila mara.


Biblia inasema katika Warumi 12:2; Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.


Mabadiliko ni matokeo ya mchakato unaoendelea wa kufanya upya akili ya mtu au nia yake. Hakuna mtu anayeza kusema amefanywa upya nia yake ikiwa anaendelea kuishi kama kawaida ya Maisha yake ya awali. Huwezi kusema nia yako au akili yako imefanywa upya kwa miaka kumi iliyopita. Hiyo sio sawa kufanywa upya kwa nia na akili ni mchakato wa kila siku na wala sio wa siku moja tu.


Hakuna mtu anayeza kusema amefanywa upya nia yake ikiwa anaendelea kuishi kama kawaida ya Maisha yake ya awali.


Kufanywa upya kwa nia zetu ni kwa Neno la Mungu. Kila mtu ambaye ameona mabadiliko ya maisha yake atakuwa na ushuhuda huu kwamba wana ushirika wa kudumu na endelevu na Neno.





Bidii ni sifa muhimu sana katika mchakato huu unaoleta mabadiliko. Kama vile divai ya jana haiwezi kuleta matokeo ya kulewa kwa aliyeinywa jana, vivyo hivyo unahitaji neno kila wakati katika Maisha yako.


2 Wakorintho 3:18 (Tafsiri kutoka AMP) inasema, sisi sote, kana kwamba kwa uso usiotiwa utaji, [kwa sababu] tuliendelea kuutazama [katika Neno la Mungu] kama vile katika kioo utukufu wa Bwana, tunageuzwa kila mara katika utukufu wake. taswira yake katika utukufu unaoongezeka daima na kutoka kiwango kimoja cha utukufu hadi kingine; [kwa maana hili] hutoka kwa Bwana [Aliye] Roho.


Mtoto wa Mungu, usikubali na usiridhike kufanywa upya kwa nia yako mara moja. Endelea kuliruhusu neno la Mungu kwenye Maisha yako kila siku.




 Tambua tu kuwa kwa kadiri unavyodumu kwenye neno lake kila siku ndivyo kadiri nia yako inazidi kuwa mpya siku zote; na kwa hayo utaweza kujua mapenzi ya Mungu kwako yaliyo mema, makamilifu na kumpendeza yeye siku zote

Haleluya!!


Itaendelea…




Wednesday, April 29, 2020

KARAMA ZA ROHONI NA UTENDAJI WAKE (Sehemu ya kwanza)


KARAMA ZA ROHONI NA UTENDAJI WAKE (Sehemu ya kwanza)
                                     NA; JAMES F. MZAVER
   



Bwana Yesu asifiwe sana niwakaribishe tena katika somo jingine la karama za Roho Mtakatifu katika maisha ya mwamini. Licha ya kua na uelewa mmbaya katika karama za rohoni pia kumekua na udanganyifu katika mafundisho ndani ya kanisa la Kristo katika swala hili, hivyo Bwana amenipa kibali niweze kuleta mfululizo wa karama za Rohoni kwanzia karama ya kwanza hadi ya mwisho na nina Imani Roho Mtakatifu atatusaidia ili tuweze kuelewa zaidi. Karibu sana


KARAMA ZA ROHONI NI NINI?
Naam kabla ya kuangalia karama zenyewe katika maandiko ni vyema kwanza tuweze kuelewa nini maana ya karama ni nini.

KARAMA ZA ROHONI ~ ni zawadi, za Roho Mtakatifu kwa kila mwamini ndani kanisa kwa lengo la kujenga kanisa na la kusaidia kazi ya Bwana itendeke.



Hizi ndizo nyenzo au vitendea kazi katika shamba la Bwana, inakua ni ngumu sana kwa mwamini au kanisa kuishi bila karama za Roho Mtakatifu ni lazima udumavu utaonekana tu.

MGAWANYO WA KARAMA ZA ROHONI
Karama za Rohoni kibiblia zipo katika makundi au mafungu mbalimbali ambayo nitaenda kukufundisha katika masomo yanayofuata moja baada ya nyingine na jinsi zinavyotenda kazi ndani ya mwamini na kanisa pia. Biblia inatufundisha juu ya karama hasa katika vitabu vya (1 Wakorintho 12:4-11 na Warumi 12:6-8) maandiko hayo yanatuonesha aina mbalimbali za karama tuanze na andiko la

1 Wakorintho 12:4-11
 Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.
Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.
Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.
Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.
Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;
mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;
10 na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;
11 lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama


Mistari hii inatuonesha kwanza mgawanyo kabla ya karama zenyewe angalia kwa makini kwanza mstari wa 4 hadi wa 6 tunaona kwanza mgawanyo wa utatu katika utendaji kazi katika kanisa au kwa mwamini mwenye huduma na vipawa. Anasema pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule na pana tofauti kati ya huduma lakini Bwana ni yeye yule na pana tofauti za utendaji kazi na Mungu ni yeye yule.

Maana yake ni hii apo juu kwanza mtoa karama ni Roho Mtakatifu na mtoa huduma ni Bwana au Yesu Kristo na anayefanya hizo zote zitende kazi katika aina mbali mbali ni Mungu Baba
Angalia;


ROHO MTAKATIFU         ___      ANATOA KARAMA
MWANA (YESU KRISTO)    ___     ANATOA HUDUMA
MUNGU BABA                ___       ANAWEZESHA UTENDAJI WOTE




Karama ambazo tumeziona sawa sawa na andiko la Wakorintho ziko karama 9 ila ziko katika mafungu makuu matatu ambazo nitazielezea kwa kina katika masomo yajayo. Karama za Roho Mtakatifu na makundi yake.

KARAMA ZA UFUNUO
1.      NENO LA MAARIFA
2.    NENO LA HEKIMA
3.     KUPAMBANUA ROHO


KARAMA ZA NGUVU
1.      IMANI
2.    MATENDO YA MIUJIZA
3.     KARAMA ZA KUPONYA


KARAMA ZA LUGHA
1.      UNABII
2.    TAFSIRI ZA LUGHA
3.     AINA ZA LUGHA


Ujumla wake ni karama tisa (9) zile zile na utendaji wake ni chini ya Roho Mtakatifu mwenyewe, Lakini bado Biblia inatufundisha Zaidi karama Zaidi ya hizi katika kitabu cha Warumi 12:6-8

Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani;
ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake;
mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.

Sawa sawa na kitabu cha Warumi 12:6-8 tunaona karama Zaidi kama vile karama ya kuonya, kukirimu, kusimamia na kurehemu. Kumbuka hizi zote ni karama za kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, haina maana kwamba watu wasio na Roho Mtakatifu hawawezi kua na hizi karama la! Mtu anaweza kua na karama bila ya mwenye karama kua pamoja naye. Naam huenda hujanielewa vizuri ngoja nikwambie Zaidi juu ya hili ni muhimu sana kuelewa. Kitabu cha Mathayo 25: 14-30 



kinaelezea juu ya talanta. Ipo siri kubwa sana juu ya hii habari hasa mistari ya mwanzo juu ya kisa hiki cha talanta. Kwanza kabisa maana ya neno talanta likimaanisha kipawa, uwezo au zawadi. Haina tofauti kabisa na maandiko yetu ya mwanzo juu ya karama za Roho Mtakatifu katika ugawanyaji wake wa karama katika maisha ya mwamini. Hebu tangalie basi mstari wa 14 na 15 wa Mathayo 25

Mathayo 25:14-15 14 Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.
15 Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.

Angalia mstari wa 15 mwishoni imeandikwa baada ya kuwagawia kila mmoja kwa uwezo wake yule Bwana akasafiri. Kiroho andiko hili liko sawa kabisa na karama za Rohoni katika kanisa. Na juu ya andiko hili tunaona mambo mawili makuu ya msingi ya kufahamu hasa kwa habari ya karama za Rohoni.


1.      Karama za Rohoni hutegemea Zaidi uwezo wako wa rohoni. Naam angalia mstari wa 15. Akampa mmoja talanta tano… kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake. Hii haimaanishi kwamba karama hutolewa kwa kigezo cha uwezo wa mtu kiroho maana sawa sawa na andilo letu la awali la Wakorintho 12 Roho mwenyewe humgawia kila ampendaye karama zake. Lakini pia Mtume Paulo anatwambia katika 1 Wakorintho 14:2 …kuhusu kutaka karama zilizo kuu, ambazo hizi huendana kabisa na uwezo wa kiroho

2.    Unaweza ukawa na karama pasipokua na yule aliyekupa karama. Naam hii ni siri nyingine katika andiko apo juu mstari wa 15 mwishoni kabisa Biblia inasema “AKASAFIRI” ikiwa na maana hawa watumwa walipewa talanta yaani karama na Bwana wao na baadaye yule Bwana akasafiri zake akawaachia karama ambazo walipaswa kuzifanyia kazi ili zizae. Ndugu kua na karama haimanishi ndio dalili ya mtu kua na Roho Mtakatifu La hasha!! Ni jambo moja kua na Roho mtakatifu kwenye maisha yako na ni jambo jingine kua na karama zake kwenye utendaji. Balaa kubwa leo kanisani ni wengi wana karama na wengi hao hao wenye karama hawana Bwana wa karama katika maisha yao wamebaki wakienda kwa uzoefu tu pasipo udhihirisho halisi wa Roho Mtakatifu katika maisha yao. Hivi leo ni jambo la kawaida kuona mkristo aliyeokoka kushindwa ata kudhihirisha utendaji kazi wa Roho Mtakatifu katika huduma.



Ndugu hayo ni mambo mawili ya msingi sana kukumbuka katika swala la karama. Karama haina matunda yeyote endapo haisukumwi na yule aliyekupa, epuka ukawaida kwa kile Mungu alichokujalia kukupa ni hatari sana
Katika kuongezea juu ya karama 9 za Roho Mtakatifu Biblia inatwambia yapo matunda 9 pia ya Roho mtakatifu ambayo kwa wakati mwingine nitayaelezea.

Lakini haya yote katika makundi yake yaani karama pamoja na matunda ya Rohoni cha umuhimu Zaidi ni kua na tunda la Roho kwanza na karama badae  Karama zote hutendeka chini ya tunda la Roho katika upendo. Ndugu umuhimu wa karama ni tunda la Roho japo zipo faida nyingi mbalimbali lakini katika upendo ndilo kuu Zaidi.

Itaendelea….
  


UBARIKIWE SANA



Imeandaliwa na kuandikwa na;       James F. Mzava
Simu namba ;                 0756259621
Barua pepe;                     jamesmzava@gmail.com





Wednesday, April 22, 2020

JIFUNZE KUWATAMBUA MANABII WA KWELI NA WA UONGO KIBIBLIA.


 JIFUNZE KUWATAMBUA MANABII WA KWELI NA WA UONGO KIBIBLIA.


                                  Na Mwl. James F. Mzava





Bwana Yesu asifiwe sana. Nipende kukukaribisha tena katika masomo haya ya kujengana kiroho, na leo Mungu amenipa kibali niweze kukuletea somo jingine juu ya manabii wa kweli na wa uongo kwa mtazamo wa kibiblia. Kwa kifupi sasa kumekua na manabii wengi ulimwenguni kote na kila ukiwauliza watakwambia wao ni manabii wa Bwana lakini wengineo hawaendani na matendo yalio sawa na nabii zao pamoja na utakatifu wa kweli. Basi fatana nami mwanzo hadi mwisho wa somo na natumaini Roho Mtakatifu atakuwezesha uweze kuelewa Zaidi.



NABII NI NANI?
Ndio ili kuweza kuelewa somo vizuri ni vyema tutambue uyu mtu nabii ni nani na ni nini chanzo chake hasa katika Biblia.
NABII ~ kiebrania neno nabii linatumika kama “nabi” na ambapo pia kiyunani linatumika kama prophetes yakiwa na maana “yeye asemaye kwa niaba/wakili” ambapo kibiblia wakijulikana kama “mwonaji”. Na hii ni kwasababu ya nguvu ya kiroho aliyonayo nabii ya kuona mambo ya kiroho yaliyopita,yaliyopo na yale yajayo kwa uwezo wa Mungu.



Na katika Biblia manabii mara nyingi wamekua watu wenye kufundisha na kutabiri juu ya kile Mungu anawaonesha kwa mambo yaliyopo na yajayo. Na ufundishaji wao ni tofauti na watumishi wengine wa Mungu kwani wao mafundisho yao yanalenga Zaidi kufundisha maonyo juu ya nabii watabirizo. (Isaya 1:4; 25:8). Na manabii hawa walikua na jukumu la kunena kwa uaminifu wote neno ambalo Mungu amemtuma Kunena wala si kwa mashauri yao wenyewe. Walikua ndio vioo kwa Israeli cha kuwaonesha Taifa lote jinsi Mungu anavowaona na ujumbe Mungu anaowapa.



Katika Biblia Zaidi ya watu 133 waliwahi kuitwa manabii wakiwemo manabii wa kike (wanawake) 16. Na wengine wa Zaidi unawaona wale mabii wazee 70 wa Israeli katika Biblia wakitabiri pia (Hesabu 11:25), Zaidi pia tunaona manabii wengine wa ziada 100 waliookolewa na Obadia (1Wafalme 18:4) nabii wa kwanza kabisa kuanza katika Biblia ni Henoko na andiko katika kitabu cha Yuda linatwambia unabii aliopewa Henoko
Yuda 1:14-15
  Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu,
15  ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake.

Mwingine ni Ibrahimu (Mwanzo 20:7) ambapo twaona ya kwamba Mungu akanena na Ebimeleki katika ndoto usiku na kumwambia kua Ibrahimu ni nabii wangu.




Na kabla hatujaendelea Zaidi ni vyema utambue kwamba huduma ya kinabii si ya mtu mwenyewe bali ni zawadi maalumu kutoka kwa Mungu (Isaya 28:10). Na hapa tunapoongelea huduma hii hatumuongelei mtu atumikaye kwayo bali tunaongelea juu ya huduma maalumu (ofisi) ambayo mtu anatumika kwayo.
Katika huduma ya kinabii ni muunganiko wa pamoja wa kusikia, kuona, kunusa, kushika na kuhisi toka kwa Bwana namaanisha milango yote ya fahamu katika mtu atumikaye kama nabii. Mungu humtumia kunena, kumuonesha, kumgusa na hata kuhisi juu ya kile anachopewa juu ya wengine kama ujumbe au unabii kwao. Nabii si mtu awezaye kuona tu kama wengine wanavyoelewa bali ni mtu mwenye uwezo huo wote hapo juu.



NGAZI ZA KINABII (WITO)
Ndiyo katika huduma hii imegawanyika pia katika ngazi sio manabii wote wanafanana uwezo na utendaji pia, nahii ni kutokana na jinsi nabii alivyopokea wito wake kwa Mungu. katika Biblia zipo ngazi kuu tatu (3) za wito wa nabii kama nabii. Ambazo ntakuorodheshea hapa na kukufafanulia kama ifuatavyo.


1)  NABII ALIYEITWA NA KUTENGWA NA MUNGU MWENYEWE.
Katika Biblia unaweza kuona kuna manabii wakubwa na wadogo pia lakini nikwambie kitu manabii hao wapo katika wito au ngazi tofauti sawa sawa na Mungu alivyowaita. Katika wito wa kinabii huu ndio wito mkubwa Zaidi maana Mungu mwenyewe humtenga mtu tangu hajazaliwa na wengineo baada ya kuzaliwa kwa kusudi maalumu la kua nabii. Ambapo hii hua ndani ya mtu kiasili tangu utoto na maisha yote ya mtu Mungu anamtumia kwa kazi moja tu ya kinabii wala sio nyingine. Yeremia ni mmojawapo wa manabii aliyeitwa na Mungu na kutengwa tangu tumboni mwa mamaye.
Yeremia 1:4-5
 Neno la Bwana lilinijia, kusema,
5 Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.

 Angalia hapa ni Mungu mwenyewe anamuweka nabii Yeremia ata kabla hajamuumba tayari alishatengwa na Mungu tumboni, nah ii inatuonesha kua ndilo kusudi lake Yeremia ambalo Mungu analidhibitisha katika andiko hapo juu ila tayari alishakua nabii kabla hata ya watu hawajaanza kumuona wala hata kabla hajazaliwa.
Manabii wa aina hii huwa na muda mwingi na Mungu sio wale wanaotumia mda mwingi na wanadamu kwa ajili ya kujionesha kama ilivo kwa manabii wengi wa sasa.
Mfano wa manabii hawa ni Yeremia, Isaya, Ezekieli Na Danieli

2)  NABII ALIYEKUJA KUWA NABII
Ndio hapa kuna mambo makubwa mawili ya kuzingatia katika aina hii ya nabii. Kwanza kabisa maana ya nabii aliyekuja kua nabii ni yule mtu ambaye mwanzoni hakua nabii alikua ni mtu wa kawaida kabisa ila baadaye anakuja kua nabii kwa kupewa karama ya kinabii au kwa kuwekewa mikono na nabii mwenye wito wa asili toka kwa Mungu ili awe nabii na ni hii hutokea hasa mahali ambapo hakuna nabii wa asili basi Roho Mtakatifu huamua kumpa mtu kipawa cha unabii ili atumike kama nabii ila awali hakua nabii
Na Biblia inaweka wazi kabisa aina za manabii hawa katika (Amosi 7:14)


AMOSI 7:14
 Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu;
Angalia andiko hilo hapo juu utaona Amosi nabii anasema kabisa yeye hakua nabii bali alikuwa ni mchungaji na mtunza mikuyu, angalia ni mtu wa kawaida kabisa ila kwa sababu ya Mungu alikosa nabii nyakati izo aliamua kumpa Amosi karama ya nabii ili aweze kutoa unabii kwa Israeli nyakati zile.



Na pia katika Wafalme tunaona nabii Elia anaamua kumpa au kumwachia karama mtu mwingine kabisa ambaye awali hakua nabii ambaye ni Elisha (2 wafalme 2:7-14) Elisha anaomba roho ya Elia iwe ndani yake ili na na yeye aweze kua kama nabii Elia na ndivyo ilivyokua kwake.
Ni vyema ukumbuke katika aina hii nabii wa kupewa karama au yule aliyekuja kuwa nabii hawezi kuzidi kiwango cha nabii yule ambaye Mungu alimtenga na kumwita tangu awali.
Katika nyakati za leo manabii wengi wapo katika aina hii za manabii maana wengi wao unaweza kuona maisha yao pamoja na nabii zao zinatofautiana sana na zile za manabii wakubwa wa apo mwanzo. Katika tafiti yangu fupi kati ya wale wanaojiita manabii katika ulimwengu huu wa sasa wengi wao hutofautiana sana na neno la Mungu hasa pindi linapokuja swala la wito au kitengo chao cha kinabii.
Mfano wa manabii hawa ni Amosi, Elisha


3)  NABII ALIYETUMWA NA MUNGU KWA UJUMBE MAALUMU
Usichanganyikiwe hapa katika maana upo utofauti kati ya yule nabii wa kwanza ambaye ameitwa na kutengwa na Mungu na yule ambaye ametumwa na Mungu juu ya watu au katika eneo Fulani.
Katika biblia aina za manabii wa aina hii ni kama Yona ambao kazi yao kubwa ni ya nyakati na nyakati namaanisha hawa hutabiri katika nyakati tofauti kulingana na jinsi Bwana alivyonena nao na kuwatuma.

Yona 1:1-3
1  Basi neno la Bwana lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,
2  Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.
3  Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa Bwana; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa Bwana.

Ukisoma kwa makini andiko ilo la kitabu cha Yona utaona utafauti mkubwa juu ya nabii huyu na unatambua si wa kundi halisi la kinabii maana kibiblia nabii halisi wa Bwana hutekeleza kile ambacho Bwana amenena naye. Ila uyu unaona Bwana anasema naye na badala ya kutekeleza na kutabiri juu ya Ninawi unaona anakimbia, kivipi?? Kwa sababu ni nabii ambaye hakua mzoefu katika karama ya unabii ni nabii ambaye Mungu humtuma tu juu ya eneo Fulani lakini si mara zote Bwana anawatumia ila hutumwa tu katika eneo Fulani juu makusudi maalumu ya Mungu

Mfano wa manabii wa aina hii ni Yona, Nathani na nabii kijana wa kitabu cha wafalme.


                                        NABII WA UONGO NI NANI
Ndio ni vyema baada ya kuangalia hapo juu aina za manabii wa kimungu ni vyema basi tukaelewa manabii wa uongo ni kinanani

NABII WA UONGO~ ni nabii yule anayechukua neno la kinabii kutoka kwenye ulimwengu wa roho kwa nguvu nyingine ambayo si ya kimungu ila ni ya kipepo kwa lengo la kuwadanganya watu.


Ngoja nikwambie neno kua nabii wa uongo si kwamba ni nabii ambaye ni anaona mambo ambayo hayapo kwenye ulimwengu wa kiroho, hapana nabii wa uongo ana uwezo wa kuona na kutabiri ila si yale yatokayo kwa Mungu ila kwa shetani. Manabii wa huongo huona sahihi ila lile neno lao la kinabii hua si sahihi namaanisha maelekezo yao huwa ni ya kipepo lenye lengo la kudanganya watu.

itaendelea .....


imeandaliwa  na kuandikwa na  JAMES F MZAVA


Mawasiliano;                    simu no; 0762759621
                                           barua pepe; jamesmzava@gmail.com







Tuesday, September 4, 2018

FAIDA ZA KUSOMA NENO LA MUNGU KATIKA MAISHA YA MWAMINI


FAIDA ZA KUSOMA NENO LA MUNGU KATIKA MAISHA YA MWAMINI

Sehemu ya kwanza (1)
Na; James F. mzaver




Bwana Yesu asifiwe nipende kuwakaribisha tena katika somo jingine linalohusu umuhimu na faida mbalimbali pindi tunapolisoma neno la Mungu. hivi leo neno la Mungu limekua kama kitu kigumu kueleweka hasa kwa waaamini wanapolisoma na hii ni kwa sababu ya kutojua umuhimu na faida za kulisoma neno. Ngoja nikwambie chochote kisichoeleweka kwa urahisi basi tambua ya kua kina urahisi kukupa matokeo chanya kama utajikita katika kujifunza hadi ukielewe, ila chochote kinachoeleweka kiurahisi ni vigumu kukupa matokeo muhimu katika maisha yako. Usisahau hii kanuni itakusaidia sana.



NINI MAANA YA NENO LA MUNGU.
Naam twende moja kwa moja katika somo letu hapo juu kabla kabisa hatujajua umuhimu na faida za neno lazima basi tuweze kuelewa maana ya neno la Mungu ni nini.


NENO LA MUNGU ~ Ni ujumbe wa kiungu kwa wanadamu wenye lengo la kuwaokoa, kuwafundisha, kuwaonya, kuwaadibisha katika makosa yao ili kuwafanya wawe wakamilifu katika Kristo.

NENO LA MUNGU~ Ni Mungu mwenyewe na ni Yesu mwenyewe, na ni uzima na uzima ni nuru yetu.


Unaposoma neno unaanza haya madaraja manne kwanzia kwa Mungu mwenyewe hadi neno linakua na manufaa kwako yani kuwa nuru yako. Na neno nuru Kiebrania limemaanishwa kama maendeleo ya watu. Yaani unapozidi kulisoma na kulijua hatima yako ni lazima uendelee kimaendeleo.


Neno la Mungu kiini chake ni kutupa uzima tulioupoteza tulipofanya dhambi, na uzima huu ni kufunuliwa kwa neno lake kwetu. Mtu anapoishi maisha ya mafunuo ya neno la Kimungu katika maisha yake ni lazima afanikiwe (NASEMA TENA NI LAZIMA AFANIKIWE)



Yaani maana yake ni hii; MUNGU=NENO=YESU=UZIMA=NURU YA WATU



Yohana 1:1-4
 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
2  Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
3  Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
4  Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.




Si hivyo tu katika Biblia zipo tafsiri mbalimbali zinazoelezea maana ya neno la Mungu na katika maandiko mengine neno la Mungu likifananisha kama vitu vingine katika lugha ya picha kama vile upanga (Waebrania 4:12), neno la Mungu kama taa (Zaburi 119:105), neno la Mungu kama Kristo Yesu (Yohana 1; 1-4), neno la Mungu kama vazi (Ufunuo 19:13) neno la Mungu kama kweli (Yohana 17; 17) na kadhalika.

Sasa katika sehemu yetu hii ya kwanza tuangalie mfano ambao Bwana Yesu aliutoa juu ya neno lake 



tuangalie (Marko 4:1-20; 21-24,35)
1  Akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari.
2  Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake,
3  Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda;
4  ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila.
5  Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba;
6  hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka.
7  Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda.
8  Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.
9  Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie.
10  Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano.
11  Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,
12  ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa.
13  Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje?
14  Mpanzi huyo hulipanda neno.
15  Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao.
16  Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha;
17  ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa.
18  Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno,
19  na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai.
20  Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.
21  Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango?
22  Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi.
23  Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.
24  Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.


Yesu anawaambia wanafunzi wake juu ya mfano wa neno la Mungu kwao, japo unakua vigumu sana kwa wanafunzi kuelewa maana ya mfano ule hadi pale Yesu alipoanza kuwafafanulia maana ya mfano wa Mbegu akiwaambia kua mbegu ni Neno la Mungu.
Lakini tujiulize swali kwa nini wanafunzi wa Yesu hawakuweza kuelewa ule mfano?

JIBU – kwa sababu neno la Mungu ni siri si kila mtu amejaliwa kutambua siri hiyo. (angalia mstari wa 11-13)


NENO LA MUNGU NI SIRI SI KILA MTU AMEJALIWA KULIELEWA, UNAPOSOMA NENO OMBA KWANZA ROHO MTAKATIFU AKUPE ROHO YA UFUNUO ILI UELEWE USIWE KAMA WANAFUNZI WA YESU WALIOSHINDWA KUELEWA (WAEFESO 1:17)



Hivyo kama neno la Mungu ni siri tambua kuokoka haitoshi na kusoma neno hakutoshi kama huna Roho ya ufunuo ili kuweza kuelewa kile ambacho kimeandikwa ili kikusaidie kuendelea.



Tambua kibiblia kwa sisi tuliokoka ili tuweze kuishi na kuenenda katika maisha haya ni lazima kila siku tupate neno jipya katika kinywa cha Bwana, vinginevyo hatuwezi kuishi na kustahimili bila neno. Biblia inasema kua neno lake ni chakula; kama vile miili yetu haiwezi kuishi bila vyakula hivyo basi tambua kua hata wewe uliyeokoka huwezi kuishi bila neno la kutosha (la kushiba) katika maisha yako. Sababu kubwa ya wakristo kurudi nyuma ni kutosoma neno, sababu kubwa ya wakristo kua na utapia mlo wa kiroho ni kwa sababu ya kutokua na neno la Mungu la kutosha katika maisha yao ivo ni rahisi kuchukuliwa katika mafundisho potovu na manyonge.


TAMBUA KILA TAARIFA UNAYOISIKIA NA KUIIFADHI NI CHAKULA.



Ndio mwanadamu ni muunganiko wa vitu vitatu; Roho, Nafsi na mwili na vyote hivi ili viishi lazima vipate chakula sahihi Roho yako ili iishi ni lazima ipate neno na muunganiko way eye aliyekuumba yaani Mungu (Yohana 4:23) inapokosa ivyo Roho yako imekufa hata kama bado unaishi kama huna neno na huna Mungu wewe ni maiti kiroho unayetembea.



Nafsi yako inahitaji taarifa sahihi zenye maarifa ili nafsi iishi lazima mtu wa Mungu uwe makini na yale unayoyasikiliza na kujifunza iwe ni kwa kuona au ata kusikia maana apo ndivyo vyakula vya nafsi yako. Kwa kadri unapozidi kusoma neno unalisha nafsi yao pia, ndani yako kunakua na uzima si wa rohoni tu hadi kwenye nafsi yako. Ila kama unajifunza mambo ya kiovu ndivyo unavyoua nafsi yako katika mambo ya Kiungu.


KADRI UNAPOSOMA NENO NDIVYO KADRI UNAZIDI KUA NA AFYA YA NAFSI YAKO PIA; UTAWAZA VYEMA, UTATOA MAAMUZI SAHIHI, NA KUA NA MIPANGO SAHIHI.



Turudi kwenye andiko letu la Marko 4 tuendelee kujifunza Zaidi juu ya neno la Mungu kwetu. Tuangalie mstari wa 33

33  Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia;




       NENO LA MUNGU LINAENDANA NA KUSIKIA



Tambua kiwango cha neno la Mungu kutenda kazi katika maisha yako kinategemeana na kiwango unachosikia.


Angalia vizuri mstari wa 33b anasema kwa kadiri walivyoweza kusikia ndivyo kadiri alivyosema nao neno lake. Sasa hutaweza kuelewa Zaidi kama sijakupeleka kwenye kitabu cha Warumi tujua uku kusikia kukoje.


Warumi 10:17   Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.


Ooh kumbe kusikia uku Yesu alikokua anakusema ni kusikia kwa njia ya Imani, inamaana Imani ni mlango unaoachilia kiwango cha neno la Mungu katika maisha yako

Inamaana mtu mwenye mafunaa juu ya neno la Mungu ni yule mwenye kiwango kikubwa cha kiimani, namaanisha kwa kadiri Imani yako ilivyo ndivyo kadiri ya kiwango utakachoelewa neno lake.



Ngoja nikwambie ni vigumu sana Mungu kusema nasi kwa sauti yake kupitia neno lake kama hatuna Imani inayotufanya kusikia.

UNAPOKOSA IMANI UNAKUA MLEMAVU WA KIROHO.

Labda hujanielewa Biblia inatwambia kua Imani ni kua na uhakika juu ya mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana (Waebrania 11:1) Unaposoma au kusikia neno la Mungu jifunze jinsi ya kujenga Imani yako ya sasa na baadaye ili neno la Mungu liweze kuzaa matunda katika maisha yako.


Turudi kwenye andiko letu la Marko 4 juu ya zile mbegu na maana zake. 

Pale tunaona maeneo manne tofauti katika mbegu ilipopandwa tuangalie maeneo hayo;

  •       kando ya njia
  • 2.     penye mwamba                    
  • 3.     penye miiba
  • 4.     penye udongo mzuri


Biblia inatwambia katika kila eneo kulikua na changamoto lakini cha ajabu wote walisikia angalia mistari ya (15, 16, 18 na 20) Biblia unatwambia kila eneo lilipopandwa mbegu  katika ufafanuzi kila mtu aliweza kusikia ila matokeo hayakua sawa.



Kwaiyo ngoja nikufundishe kitu hapa kusikia tu haitoshi ni hatua ya mwanzo ya  neno la Mungu na hapa shetani anaweza kukurusu ukasikia lakini asikupe nafasi ya kukuza kile ambacho umekisikia. Mbegu inaweza kupandwa na shetani asikusumbue kupandwa kwa ile mbegu ila shida yake ni kuangalia eneo ambapo mbegu imepandwa kama ni kwenye udongo mzuri shetani huleta vita ili kusudi akuhamishe katika miba, mwamba na kwenye njia ili usiweze kuzaa matunda ya neno na hata kama ukizaa basi uzae kwa kiwango pungufu.


TAMBUA ILI MBEGU AU NENO LA MUNGU LIWEZE KUZAA NI LAZIMA UWE KATIKA ENEO SAHIHI


Tambua eneo sahihi hapa ni mazingira pale unapolipokea lile neno kunategemeana sana na eneo unapolishwa, unapolipokea na kulisoma neno. Mazingira ayo yakiwa si sahihi tambu hutaweza kuzaa au kuona manufaa ya neno katika maisha yako na hata kama ukiyaona utayaona kwa kiwango kidogo sana.



                                UBARIKIWE SANA !!




Itaendelea



IMEANDIKWA NA KUANDALIWA NA;    JAMES F. MZAVER

MAWASILIANO;                               0762759621

BARUA PEPE;                                 Jamesmzava@gmail.com






AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)

http://bit.ly/3JGDJ4d MWL. JAMES F. MZAVER Minister Truth 0762759621 jamesmzava@gmail.com              AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1) Ukuaji ha...