Tuesday, June 13, 2017

JIFUNZE JINSI YA KUPAMBANA NA MAWAZO MABAYA NDANI YA MOYO WAKO

JIFUNZE JINSI YA KUPAMBANA NA MAWAZO MABAYA NDANI YA MOYO WAKO
                                                      NA; JAMES F. MNZAVA





Bwana Yesu asifiwe sana. Nipende kukukaribisha tena katika somo jingine la jinsi ya kupambana na mawazo mabaya ndani ya moyo wako. Ni somo ambalo nina Imani litabadilisha maisha yako kwa kiasi kikubwa. Biblia inatwambia kwamba awazavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo, je wewe umekua ukiwaza mawazo ya aina gani je wajua mawazo yako ndio wewe mwenyewe? Je wajua ulivyo sasa ni kutokana na mawazo yako uliyokua ukiwaza kabla na sasa? Basi fatana nami katika somo hili na naimani litabadili maisha yako. Karibu sana


NINI MAANA YA MAWAZO        
Ndio kwanza kabisa nipende kuanza kuelezea maana halisi ya mawazo ni nini hasa

MAWAZO ~ Ni fikra na mitazamo zinazotolewa katika akili ya mtu kwa kufikiri mambo yaliyopita, mambo ya sasa na ya badae.

Japokua mawazo hutolewa katika akili ya mtu lakini huhifadhiwa katika moyo wake na ndiko mawazo yanakoishi huko. Akili hutua tu wazo lakini kazi kubwa ipo katika moyo wa mwanadamu katika kuamua na kutekeleza mawazo hayo.

                   MAWAZO YAKO NDIO UHALISIA WAKO

Nia kubwa ya mawazo katika maisha yetu ni kutafuta jibu juu ya yale mambo yanayoonekana magumu kwetu kwa kutumia uwezo wetu wa kimawazo tuliyopewa na Mungu tuweze kuyapatia majibu.




Nikwambie kwamba mawazo yako yanaumuhimu sana katika maisha yako kama utakua namna ya kuuweka moyo wako vizuri ili uweze kuwaza mawazo ya kumpendeza Mungu.
Hebu sasa twende katika maandiko tuangalie jinsi maandiko yanasema nini juu ya mawazo ya mwanadamu.
Mithali 23:7
 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe.

Neno aonavyo katika tafsiri ya (new king james version) NKJV limeandikwa awazavyo moyoni mwake, maneno haya katika biblia yakimaanisha kua jinsi unavyowaza ndani ndani ya moyo wako ndivyo ulivyo.
Mawazo ndiyo yanayakufanya wewe uwe katika ulimwengu huu tunaoishi. Hivyo ulivo sasa ni matokeo tu ya moyo wako umejaza mawazo gani.
Ngoja nikwambie hakuna kitu cha kulinda katika maisha yako vizuri kama moyo ulio ndani yako maana ndio hazina ya mawazo yako, ndilo chimbuko biblia inatwambia haya katika kitabu cha mithali


Mithali 4:23
 Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
Ninaweza kusema kutokana na andiko hili tukiliweka pamoja na lile andiko la Mithali 23 tunapata kitu kikubwa Zaidi cha kujifunza tunaona kwamba jinsi mawazo yako yalivyo ndivyo ulivyo wewe kadhalika na katika kujiona huku ndani yako kuna chemchemi za uzima sasa inategemea unachowaza je ni uzima au ufu.


MAWAZO YAKO YANAWEZA YAKAZAA UZIMA AU UFU
Ndio ngoja nikwambie kama biblia inatwambia kwamba moyo ndani yake ndiko mawazo huwazwa na ndani ya moyo huo huo ndiko chemchemi za uzima zilipo basi ni wazi kua chemchemi hizi zinategemeana sana na kuwaza kwako. Na hatuna budi kuomba kibali kama alichokiomba Daudi mawazo yetu yapate kibali yaani yapate neema ili kuendelea kutunza chemchem za uzima ndani yetu.
Kupitia maandiko haya unaweza kuona mawazo mabaya huharibu maisha yetu na kuharibu uzima uliondani yetu. Na tunachojifunza hapa Zaidi ni kwamba kwa mawazo tu siku zetu zinaweza kufupishwa au kuendela kuongezwa kwa kuendelea kuomba maombi ya kibali kwa kila unachowaza.
Kua makini mpendwa kwa maana kwa kushindwa kulinda mioyo yetu tunamtenda Mungu dhambi mara mbili tukianza katika mioyo yetu pamoja na matendo yetu. Hebu angalia Yesu alipokua akihubiria makutano  na kuwambia kwa kuwaza tu vibaya basi mbele zake unahesabika ushatenda ata kama hujatenda katika mwili wako
Mathayo 5:27-28
 Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;
28  lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

Moyo ndio eneo kubwa la mapambano kati yetu na ibilisi hutuletea mawazo mabaya ili tushindwe kutimiza neno la Mungu katika maisha yetu. Watu wengi hudhani huhesabiwa dhambi kwa matendo yao lakini hawatambua ata kwa mawazo yao kua mabaya ni dhambi kama dhambi nyinginezo na zinahitaji toba ya kweli kabisa mbele za Mungu. Hebu jiulize sasa ni mara ngapi umeomba toba juu ya mawazo yako kua mabaya moyoni mwako je umetamani je umemwazia mwenzako vibaya? Tambua fika kwamba umefanya dhambi na unahitaji toba na msamaha wa Mungu kwako.


VITA VYETU KIROHO HUANZIA KWANZA KWENYE MAWAZO YETU


Ndio hii ndio mbinu kubwa sana ya shetani ya kuwashinda waumini kwa kuwaletea mawazo mabaya katika mioyo yao, kwa kuanza kuwakumbusha mambo ya nyuma na yasioyofaa katika mioyo yao kwa nia ya kuwaharibu Imani zao kwa Mungu ili wasikubalike na Mungu.
Nikwambie kitu kupitia mawazo mabaya yanafanya moyo wako unajisike na kukosa mwelekeo wa kumtafuta Bwana kwa roho na kweli mara zote unakuta mtu anakua vuguvugu tu wa kuanguka na kuinuka kwa sababu ya kushindwa namna ya kuendesha mawazo yake katika njia ya Bwana.




Biblia inatwambia kwamba kabla hatujaingia katika maombi ya kivita ni lazima tuhakikishe tunapambana kwanza na mawazo yasiyotokana na Mungu ili kuweza kupata ushindi katika vita vyetu.

2 wakorintho 10:4

 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;

kumbuka kabisa kabla hujaingia katika maombi yako ya kuomba ahadi za Mungu kwako ni lazima uanze kupambana na mawazo yote yanayojiinua kinyume na kusudi la Mungu katika maisha yako na utauona mkono wa Bwana ukitenda sana katika maisha yako.

Lakini pia mawazo mabaya hutujia kila muda katika maisha yetu jifunze kupambana nayo kiroho hapo hapo ili kutokaa na sumu ya mawazo ya adui itakuharibu jifunze kuomba kiroho na kuomba ndani ya moyo wako katika kuyapinga mawazo haya mabaya.

                       Dhambi huja kwa mawazo

Ndio shetani apohitaji kumuingiza mtu kwenye dhambi yeyote humpa kwanza wazo juu ya dhambi hiyo na mawazo hayo ya kidanganyifu huyaremba ndani ya moyo wake na baada ya kushawishika mtu huanguka katika dhambi angalia (Yakobo 1:13)

Yakobo 1:13-14

 Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.
14  Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.

biblia inatwambia mtu hujaribiwa kwa kuvutwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa kwa kudanganywa, na njia ambayo shetani huitumia kumvuta mtu kuanguka ni kupitia mawazo yake. Angalia sana jinsi uwazavyo na jifunze kuomba maana mawazo ni mlango mojawapo wa dhambi kuingia katika maisha ya mtu.



Na kabla sijaendelea mbele Zaidi mwanadamu kama mwanadamu katika mawazo yake yamegawanyika katika aina kuu  mbili

®Mawazo yenye kibali (mema)
®Mawazo yasio na kibali (mabaya)

Mawazo yenye kibali ni yale yanayompendeza Mungu. Ndio maana daudi anaandika kuhusu ilo katika (zaburi 19:14)
Zaburi 19:14
  Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.

Daudi anasema kwamba mawazo ya moyo wake yapate kibali, yaani yawe mema mbele za Mungu kwa maana alitambua kama ungewaza vibaya katika maisha yake basi angekosa kibali mbele za Mungu.
Nipende kukwambia maana ya maneno haya katika zaburi hii ni kwamba mtu yeyote yule ambaye anawaza mawazo mabaya basi huwa mbali na Mungu na kukosa kibali kwake hatima yake ni kuangamia. Angalia sana mawazo yako maana kwayo ndiyo yatakayokuwezesha kupata kibali kwa Mungu au kukataliwa na Bwana.

MAWAZO MEMA HUKUPA KIBALI MBELE ZA MUNGU

              NB: maana ya kupata kibali ni kupata neema.

Lakini pia aina ya pili ya mawazo ya mwanadamu ni yale ya upotevu yaliteyo adhabu ya Mungu kwa kua ni mabaya. Na maandiko matakatifu yanatwambia katika kitabu cha mwanzo

Mwanzo 6:5-8

Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.
6  Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.
7  Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya.
8  Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.


Biblia inatwambia kwamba pamoja na Mungu kumuumba mwanadamu na kumpa kila kitu katika dunia bado mwanadamu alimuasi Mungu. Na moja kati ya mambo yaliyomchukiza Mungu wakati huo wa Nuhu ni mioyoni mwa wanadamu kulikua na mawazo mabaya na sio siku moja bali ni siku zote za maisha yao walikua wakiwaza mawazo mabaya. Jambo lilimfanya Mungu kujua ata kumuumba mwanadamu. Hebu angalia maneno haya angalia nguvu iliyo ndani yako na jinsi unavyowaza, watu hawa waliwaza mabaya ndipo Mungu akaamua kuwaangamiza kwa gharika.

Lakini katika mstari wa nane biblia inasema kwamba Nuhu alipata kibali machoni pa Bwana yaani likimaanisha Nuhu mawazo yake yalipata kibali kwa kua mema ndipo akaokoka yeye na wanawe.


MAWAZO MABAYA HUMFANYA MUNGU KUGHAHIRI AHADI NA BARAKA ZAKE KWAKO.



Lakini jambo jingine linaloonekana hapa ni Mungu kujuta na kughahiri kwa nini alimuumba mwanadamu kwa sababu ya maovu yake kua mengi pamoja na mawazo yake ambayo ni mabaya kila siku. Mtu wa Mungu hebu angalia hapa kwa makini mawazo tu yalimfanya Mungu kughahiri ata zile Baraka na maisha ya wanadamu kwa kua yalikua mabaya.

Hebu jikagua sasa katika moyo wako je una mawazo mabaya? Au je wewe ni mtu wa kuwaza mabaya moyoni mwako? Tambua ya kwamba unajiondoshea mwenyewe Baraka zako na unamfanya Mungu asikupe kile alichokuahidia hapo mwanzo.


JINSI YA KUSHINDA MAWAZO MABAYA

1.      Weka neno la Mungu la kutosha katika moyo wako
Ndio iyo ndiyo silaha kubwa ya kupambana na mishale ya adui anayoileta katika maisha yetu kupitia mawazo. (Mathayo 4) biblia inatwambia hapa jinsi Yesu aliweza kumshinda shetani kwa neno lililokua moyoni mwake.
Zaburi 119:11
 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
Daudi anasema kwamba moyoni mwake ameliweka neno la mungu ili asimtende Mungu dhambi ndivyo nasi tunatakiwa tulijaze neno la Bwana katika mioyo yetu ili kuziba mianya ya mawazo mabaya katika maisha yetu.

2.     Ishi ukimtegemea Roho Mtakatifu hasa katika kutafuta nguvu zake wakati wa maombi.
Ndio ili uweze kushinda mawazo mabaya ya mwovu ni vyema uweke tegemea lako kwa Roho wa Mungu ili aweze kukuwezesha pindi pale shetani anapojaribu kupambana na wewe kwa njia ya mawazo mabaya ndani ya moyo wako (Mathayo 26:41) ishi ukijua ukitegemea akili zako mwenyewe utashindwa jifunze kuweke tegemeo lako kwake. (Mithali 28:26, Yeremia17:9, Mathayo 26:33)

3.     Jifunze kuulisha moyo wako kwa kumtaka Bwana pamoja na kumwangalia yeye kwa njia ya maombi.
Ndio ili uweze kushinda basi huna budi kulisha moyo wako neno la Bwana pamoja na maombi ili shetani akose nafasi katika maisha yako. Biblia inasema Ayubu aliweza kushinda tamaa zitakazomwangusha katika dhambi kwa kuamua kuweka agano na macho yake ili asivutwe katika mawazo mabaya ambayo yatamwangusha katika dhambi (Ayubu 31:1)

4.     Jitenge na vyanzo vya mawazo mabaya
Ndio watu wengi wamekua wakianguka katika dhambi baada ya wao wenyewe kukubali kuingia wenyewe katika majaribu kwa kuvutwa na tamaa zao wenyewe pasipo kuangalia mazingira wanayoishi kwamba ni hatarishi katika kumwasi Mungu. Jifunze kujitenga na vyanzo vya mazingira ambayo kila siku zinakuzalia mawazo mabaya kwa mfano vipindi vichafu vya television (phonography), picha chafu, maongeze mabaya pamoja na mengine mengi yatokanayo na hayo. Zaidi jikite katika kulitafakari neno la Bwana maana hapo ndipo mafanikio yako yalipo. (Yoshua 1:10)

5.     Tafakari neno la Mungu na epuka uvivu.
Biblia inatwambia kwamba unapolitafakari neno la Bwana ndipo tutakapofanikisha njia zetu. Hivyo ili tuwe wana wa Mungu wenye kibali kwake na mawazo yetu yakubalike kwake ni lazima kuwe na msingi wa neno la Bwana katika maisha yetu ya kila siku. Zipo faida nyingi sana katika kulitafakari neno la Bwana katika maisha yetu. Lakini pia epuka uvivu maana ndioo chanzo kikubwa pia cha shetani kuweka na kupandikiza mawazo mabaya katika mioyo yetu. Hebu angalia jinsi mfalme Daudi alipoanguka katika dhambi ya uzinzi kwa ajili ya kutega kazi na kwenda kuvutwa katika dhambi ya uzinzi.

MUNGU AKUBARIKI KWA KUSOMA.


Imeandaliwa n
a kuandikwa na;                 JAMES F.MZAVA


Mawasiliano;       0762759621, 0653194411, 0625782324


                              jamesmzava@gmail.com 
















                                                                                           

No comments:

Post a Comment

AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)

http://bit.ly/3JGDJ4d MWL. JAMES F. MZAVER Minister Truth 0762759621 jamesmzava@gmail.com              AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1) Ukuaji ha...