Wednesday, April 29, 2020

KARAMA ZA ROHONI NA UTENDAJI WAKE (Sehemu ya kwanza)


KARAMA ZA ROHONI NA UTENDAJI WAKE (Sehemu ya kwanza)
                                     NA; JAMES F. MZAVER
   



Bwana Yesu asifiwe sana niwakaribishe tena katika somo jingine la karama za Roho Mtakatifu katika maisha ya mwamini. Licha ya kua na uelewa mmbaya katika karama za rohoni pia kumekua na udanganyifu katika mafundisho ndani ya kanisa la Kristo katika swala hili, hivyo Bwana amenipa kibali niweze kuleta mfululizo wa karama za Rohoni kwanzia karama ya kwanza hadi ya mwisho na nina Imani Roho Mtakatifu atatusaidia ili tuweze kuelewa zaidi. Karibu sana


KARAMA ZA ROHONI NI NINI?
Naam kabla ya kuangalia karama zenyewe katika maandiko ni vyema kwanza tuweze kuelewa nini maana ya karama ni nini.

KARAMA ZA ROHONI ~ ni zawadi, za Roho Mtakatifu kwa kila mwamini ndani kanisa kwa lengo la kujenga kanisa na la kusaidia kazi ya Bwana itendeke.



Hizi ndizo nyenzo au vitendea kazi katika shamba la Bwana, inakua ni ngumu sana kwa mwamini au kanisa kuishi bila karama za Roho Mtakatifu ni lazima udumavu utaonekana tu.

MGAWANYO WA KARAMA ZA ROHONI
Karama za Rohoni kibiblia zipo katika makundi au mafungu mbalimbali ambayo nitaenda kukufundisha katika masomo yanayofuata moja baada ya nyingine na jinsi zinavyotenda kazi ndani ya mwamini na kanisa pia. Biblia inatufundisha juu ya karama hasa katika vitabu vya (1 Wakorintho 12:4-11 na Warumi 12:6-8) maandiko hayo yanatuonesha aina mbalimbali za karama tuanze na andiko la

1 Wakorintho 12:4-11
 Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.
Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.
Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.
Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.
Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;
mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;
10 na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;
11 lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama


Mistari hii inatuonesha kwanza mgawanyo kabla ya karama zenyewe angalia kwa makini kwanza mstari wa 4 hadi wa 6 tunaona kwanza mgawanyo wa utatu katika utendaji kazi katika kanisa au kwa mwamini mwenye huduma na vipawa. Anasema pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule na pana tofauti kati ya huduma lakini Bwana ni yeye yule na pana tofauti za utendaji kazi na Mungu ni yeye yule.

Maana yake ni hii apo juu kwanza mtoa karama ni Roho Mtakatifu na mtoa huduma ni Bwana au Yesu Kristo na anayefanya hizo zote zitende kazi katika aina mbali mbali ni Mungu Baba
Angalia;


ROHO MTAKATIFU         ___      ANATOA KARAMA
MWANA (YESU KRISTO)    ___     ANATOA HUDUMA
MUNGU BABA                ___       ANAWEZESHA UTENDAJI WOTE




Karama ambazo tumeziona sawa sawa na andiko la Wakorintho ziko karama 9 ila ziko katika mafungu makuu matatu ambazo nitazielezea kwa kina katika masomo yajayo. Karama za Roho Mtakatifu na makundi yake.

KARAMA ZA UFUNUO
1.      NENO LA MAARIFA
2.    NENO LA HEKIMA
3.     KUPAMBANUA ROHO


KARAMA ZA NGUVU
1.      IMANI
2.    MATENDO YA MIUJIZA
3.     KARAMA ZA KUPONYA


KARAMA ZA LUGHA
1.      UNABII
2.    TAFSIRI ZA LUGHA
3.     AINA ZA LUGHA


Ujumla wake ni karama tisa (9) zile zile na utendaji wake ni chini ya Roho Mtakatifu mwenyewe, Lakini bado Biblia inatufundisha Zaidi karama Zaidi ya hizi katika kitabu cha Warumi 12:6-8

Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani;
ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake;
mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.

Sawa sawa na kitabu cha Warumi 12:6-8 tunaona karama Zaidi kama vile karama ya kuonya, kukirimu, kusimamia na kurehemu. Kumbuka hizi zote ni karama za kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, haina maana kwamba watu wasio na Roho Mtakatifu hawawezi kua na hizi karama la! Mtu anaweza kua na karama bila ya mwenye karama kua pamoja naye. Naam huenda hujanielewa vizuri ngoja nikwambie Zaidi juu ya hili ni muhimu sana kuelewa. Kitabu cha Mathayo 25: 14-30 



kinaelezea juu ya talanta. Ipo siri kubwa sana juu ya hii habari hasa mistari ya mwanzo juu ya kisa hiki cha talanta. Kwanza kabisa maana ya neno talanta likimaanisha kipawa, uwezo au zawadi. Haina tofauti kabisa na maandiko yetu ya mwanzo juu ya karama za Roho Mtakatifu katika ugawanyaji wake wa karama katika maisha ya mwamini. Hebu tangalie basi mstari wa 14 na 15 wa Mathayo 25

Mathayo 25:14-15 14 Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.
15 Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.

Angalia mstari wa 15 mwishoni imeandikwa baada ya kuwagawia kila mmoja kwa uwezo wake yule Bwana akasafiri. Kiroho andiko hili liko sawa kabisa na karama za Rohoni katika kanisa. Na juu ya andiko hili tunaona mambo mawili makuu ya msingi ya kufahamu hasa kwa habari ya karama za Rohoni.


1.      Karama za Rohoni hutegemea Zaidi uwezo wako wa rohoni. Naam angalia mstari wa 15. Akampa mmoja talanta tano… kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake. Hii haimaanishi kwamba karama hutolewa kwa kigezo cha uwezo wa mtu kiroho maana sawa sawa na andilo letu la awali la Wakorintho 12 Roho mwenyewe humgawia kila ampendaye karama zake. Lakini pia Mtume Paulo anatwambia katika 1 Wakorintho 14:2 …kuhusu kutaka karama zilizo kuu, ambazo hizi huendana kabisa na uwezo wa kiroho

2.    Unaweza ukawa na karama pasipokua na yule aliyekupa karama. Naam hii ni siri nyingine katika andiko apo juu mstari wa 15 mwishoni kabisa Biblia inasema “AKASAFIRI” ikiwa na maana hawa watumwa walipewa talanta yaani karama na Bwana wao na baadaye yule Bwana akasafiri zake akawaachia karama ambazo walipaswa kuzifanyia kazi ili zizae. Ndugu kua na karama haimanishi ndio dalili ya mtu kua na Roho Mtakatifu La hasha!! Ni jambo moja kua na Roho mtakatifu kwenye maisha yako na ni jambo jingine kua na karama zake kwenye utendaji. Balaa kubwa leo kanisani ni wengi wana karama na wengi hao hao wenye karama hawana Bwana wa karama katika maisha yao wamebaki wakienda kwa uzoefu tu pasipo udhihirisho halisi wa Roho Mtakatifu katika maisha yao. Hivi leo ni jambo la kawaida kuona mkristo aliyeokoka kushindwa ata kudhihirisha utendaji kazi wa Roho Mtakatifu katika huduma.



Ndugu hayo ni mambo mawili ya msingi sana kukumbuka katika swala la karama. Karama haina matunda yeyote endapo haisukumwi na yule aliyekupa, epuka ukawaida kwa kile Mungu alichokujalia kukupa ni hatari sana
Katika kuongezea juu ya karama 9 za Roho Mtakatifu Biblia inatwambia yapo matunda 9 pia ya Roho mtakatifu ambayo kwa wakati mwingine nitayaelezea.

Lakini haya yote katika makundi yake yaani karama pamoja na matunda ya Rohoni cha umuhimu Zaidi ni kua na tunda la Roho kwanza na karama badae  Karama zote hutendeka chini ya tunda la Roho katika upendo. Ndugu umuhimu wa karama ni tunda la Roho japo zipo faida nyingi mbalimbali lakini katika upendo ndilo kuu Zaidi.

Itaendelea….
  


UBARIKIWE SANA



Imeandaliwa na kuandikwa na;       James F. Mzava
Simu namba ;                 0756259621
Barua pepe;                     jamesmzava@gmail.com





1 comment:

  1. Barikiwa sana Mtumishi wa Mungu.. hapa kuna Vitu nimejifunza.
    Pls, naweza kupata mwendelezo wa hili somo?

    ReplyDelete

AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)

http://bit.ly/3JGDJ4d MWL. JAMES F. MZAVER Minister Truth 0762759621 jamesmzava@gmail.com              AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1) Ukuaji ha...