Wednesday, April 22, 2020

JIFUNZE KUWATAMBUA MANABII WA KWELI NA WA UONGO KIBIBLIA.


 JIFUNZE KUWATAMBUA MANABII WA KWELI NA WA UONGO KIBIBLIA.


                                  Na Mwl. James F. Mzava





Bwana Yesu asifiwe sana. Nipende kukukaribisha tena katika masomo haya ya kujengana kiroho, na leo Mungu amenipa kibali niweze kukuletea somo jingine juu ya manabii wa kweli na wa uongo kwa mtazamo wa kibiblia. Kwa kifupi sasa kumekua na manabii wengi ulimwenguni kote na kila ukiwauliza watakwambia wao ni manabii wa Bwana lakini wengineo hawaendani na matendo yalio sawa na nabii zao pamoja na utakatifu wa kweli. Basi fatana nami mwanzo hadi mwisho wa somo na natumaini Roho Mtakatifu atakuwezesha uweze kuelewa Zaidi.



NABII NI NANI?
Ndio ili kuweza kuelewa somo vizuri ni vyema tutambue uyu mtu nabii ni nani na ni nini chanzo chake hasa katika Biblia.
NABII ~ kiebrania neno nabii linatumika kama “nabi” na ambapo pia kiyunani linatumika kama prophetes yakiwa na maana “yeye asemaye kwa niaba/wakili” ambapo kibiblia wakijulikana kama “mwonaji”. Na hii ni kwasababu ya nguvu ya kiroho aliyonayo nabii ya kuona mambo ya kiroho yaliyopita,yaliyopo na yale yajayo kwa uwezo wa Mungu.



Na katika Biblia manabii mara nyingi wamekua watu wenye kufundisha na kutabiri juu ya kile Mungu anawaonesha kwa mambo yaliyopo na yajayo. Na ufundishaji wao ni tofauti na watumishi wengine wa Mungu kwani wao mafundisho yao yanalenga Zaidi kufundisha maonyo juu ya nabii watabirizo. (Isaya 1:4; 25:8). Na manabii hawa walikua na jukumu la kunena kwa uaminifu wote neno ambalo Mungu amemtuma Kunena wala si kwa mashauri yao wenyewe. Walikua ndio vioo kwa Israeli cha kuwaonesha Taifa lote jinsi Mungu anavowaona na ujumbe Mungu anaowapa.



Katika Biblia Zaidi ya watu 133 waliwahi kuitwa manabii wakiwemo manabii wa kike (wanawake) 16. Na wengine wa Zaidi unawaona wale mabii wazee 70 wa Israeli katika Biblia wakitabiri pia (Hesabu 11:25), Zaidi pia tunaona manabii wengine wa ziada 100 waliookolewa na Obadia (1Wafalme 18:4) nabii wa kwanza kabisa kuanza katika Biblia ni Henoko na andiko katika kitabu cha Yuda linatwambia unabii aliopewa Henoko
Yuda 1:14-15
  Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu,
15  ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake.

Mwingine ni Ibrahimu (Mwanzo 20:7) ambapo twaona ya kwamba Mungu akanena na Ebimeleki katika ndoto usiku na kumwambia kua Ibrahimu ni nabii wangu.




Na kabla hatujaendelea Zaidi ni vyema utambue kwamba huduma ya kinabii si ya mtu mwenyewe bali ni zawadi maalumu kutoka kwa Mungu (Isaya 28:10). Na hapa tunapoongelea huduma hii hatumuongelei mtu atumikaye kwayo bali tunaongelea juu ya huduma maalumu (ofisi) ambayo mtu anatumika kwayo.
Katika huduma ya kinabii ni muunganiko wa pamoja wa kusikia, kuona, kunusa, kushika na kuhisi toka kwa Bwana namaanisha milango yote ya fahamu katika mtu atumikaye kama nabii. Mungu humtumia kunena, kumuonesha, kumgusa na hata kuhisi juu ya kile anachopewa juu ya wengine kama ujumbe au unabii kwao. Nabii si mtu awezaye kuona tu kama wengine wanavyoelewa bali ni mtu mwenye uwezo huo wote hapo juu.



NGAZI ZA KINABII (WITO)
Ndiyo katika huduma hii imegawanyika pia katika ngazi sio manabii wote wanafanana uwezo na utendaji pia, nahii ni kutokana na jinsi nabii alivyopokea wito wake kwa Mungu. katika Biblia zipo ngazi kuu tatu (3) za wito wa nabii kama nabii. Ambazo ntakuorodheshea hapa na kukufafanulia kama ifuatavyo.


1)  NABII ALIYEITWA NA KUTENGWA NA MUNGU MWENYEWE.
Katika Biblia unaweza kuona kuna manabii wakubwa na wadogo pia lakini nikwambie kitu manabii hao wapo katika wito au ngazi tofauti sawa sawa na Mungu alivyowaita. Katika wito wa kinabii huu ndio wito mkubwa Zaidi maana Mungu mwenyewe humtenga mtu tangu hajazaliwa na wengineo baada ya kuzaliwa kwa kusudi maalumu la kua nabii. Ambapo hii hua ndani ya mtu kiasili tangu utoto na maisha yote ya mtu Mungu anamtumia kwa kazi moja tu ya kinabii wala sio nyingine. Yeremia ni mmojawapo wa manabii aliyeitwa na Mungu na kutengwa tangu tumboni mwa mamaye.
Yeremia 1:4-5
 Neno la Bwana lilinijia, kusema,
5 Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.

 Angalia hapa ni Mungu mwenyewe anamuweka nabii Yeremia ata kabla hajamuumba tayari alishatengwa na Mungu tumboni, nah ii inatuonesha kua ndilo kusudi lake Yeremia ambalo Mungu analidhibitisha katika andiko hapo juu ila tayari alishakua nabii kabla hata ya watu hawajaanza kumuona wala hata kabla hajazaliwa.
Manabii wa aina hii huwa na muda mwingi na Mungu sio wale wanaotumia mda mwingi na wanadamu kwa ajili ya kujionesha kama ilivo kwa manabii wengi wa sasa.
Mfano wa manabii hawa ni Yeremia, Isaya, Ezekieli Na Danieli

2)  NABII ALIYEKUJA KUWA NABII
Ndio hapa kuna mambo makubwa mawili ya kuzingatia katika aina hii ya nabii. Kwanza kabisa maana ya nabii aliyekuja kua nabii ni yule mtu ambaye mwanzoni hakua nabii alikua ni mtu wa kawaida kabisa ila baadaye anakuja kua nabii kwa kupewa karama ya kinabii au kwa kuwekewa mikono na nabii mwenye wito wa asili toka kwa Mungu ili awe nabii na ni hii hutokea hasa mahali ambapo hakuna nabii wa asili basi Roho Mtakatifu huamua kumpa mtu kipawa cha unabii ili atumike kama nabii ila awali hakua nabii
Na Biblia inaweka wazi kabisa aina za manabii hawa katika (Amosi 7:14)


AMOSI 7:14
 Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu;
Angalia andiko hilo hapo juu utaona Amosi nabii anasema kabisa yeye hakua nabii bali alikuwa ni mchungaji na mtunza mikuyu, angalia ni mtu wa kawaida kabisa ila kwa sababu ya Mungu alikosa nabii nyakati izo aliamua kumpa Amosi karama ya nabii ili aweze kutoa unabii kwa Israeli nyakati zile.



Na pia katika Wafalme tunaona nabii Elia anaamua kumpa au kumwachia karama mtu mwingine kabisa ambaye awali hakua nabii ambaye ni Elisha (2 wafalme 2:7-14) Elisha anaomba roho ya Elia iwe ndani yake ili na na yeye aweze kua kama nabii Elia na ndivyo ilivyokua kwake.
Ni vyema ukumbuke katika aina hii nabii wa kupewa karama au yule aliyekuja kuwa nabii hawezi kuzidi kiwango cha nabii yule ambaye Mungu alimtenga na kumwita tangu awali.
Katika nyakati za leo manabii wengi wapo katika aina hii za manabii maana wengi wao unaweza kuona maisha yao pamoja na nabii zao zinatofautiana sana na zile za manabii wakubwa wa apo mwanzo. Katika tafiti yangu fupi kati ya wale wanaojiita manabii katika ulimwengu huu wa sasa wengi wao hutofautiana sana na neno la Mungu hasa pindi linapokuja swala la wito au kitengo chao cha kinabii.
Mfano wa manabii hawa ni Amosi, Elisha


3)  NABII ALIYETUMWA NA MUNGU KWA UJUMBE MAALUMU
Usichanganyikiwe hapa katika maana upo utofauti kati ya yule nabii wa kwanza ambaye ameitwa na kutengwa na Mungu na yule ambaye ametumwa na Mungu juu ya watu au katika eneo Fulani.
Katika biblia aina za manabii wa aina hii ni kama Yona ambao kazi yao kubwa ni ya nyakati na nyakati namaanisha hawa hutabiri katika nyakati tofauti kulingana na jinsi Bwana alivyonena nao na kuwatuma.

Yona 1:1-3
1  Basi neno la Bwana lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,
2  Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.
3  Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa Bwana; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa Bwana.

Ukisoma kwa makini andiko ilo la kitabu cha Yona utaona utafauti mkubwa juu ya nabii huyu na unatambua si wa kundi halisi la kinabii maana kibiblia nabii halisi wa Bwana hutekeleza kile ambacho Bwana amenena naye. Ila uyu unaona Bwana anasema naye na badala ya kutekeleza na kutabiri juu ya Ninawi unaona anakimbia, kivipi?? Kwa sababu ni nabii ambaye hakua mzoefu katika karama ya unabii ni nabii ambaye Mungu humtuma tu juu ya eneo Fulani lakini si mara zote Bwana anawatumia ila hutumwa tu katika eneo Fulani juu makusudi maalumu ya Mungu

Mfano wa manabii wa aina hii ni Yona, Nathani na nabii kijana wa kitabu cha wafalme.


                                        NABII WA UONGO NI NANI
Ndio ni vyema baada ya kuangalia hapo juu aina za manabii wa kimungu ni vyema basi tukaelewa manabii wa uongo ni kinanani

NABII WA UONGO~ ni nabii yule anayechukua neno la kinabii kutoka kwenye ulimwengu wa roho kwa nguvu nyingine ambayo si ya kimungu ila ni ya kipepo kwa lengo la kuwadanganya watu.


Ngoja nikwambie neno kua nabii wa uongo si kwamba ni nabii ambaye ni anaona mambo ambayo hayapo kwenye ulimwengu wa kiroho, hapana nabii wa uongo ana uwezo wa kuona na kutabiri ila si yale yatokayo kwa Mungu ila kwa shetani. Manabii wa huongo huona sahihi ila lile neno lao la kinabii hua si sahihi namaanisha maelekezo yao huwa ni ya kipepo lenye lengo la kudanganya watu.

itaendelea .....


imeandaliwa  na kuandikwa na  JAMES F MZAVA


Mawasiliano;                    simu no; 0762759621
                                           barua pepe; jamesmzava@gmail.com







No comments:

Post a Comment

AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)

http://bit.ly/3JGDJ4d MWL. JAMES F. MZAVER Minister Truth 0762759621 jamesmzava@gmail.com              AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1) Ukuaji ha...