Tuesday, June 13, 2017

JIFUNZE JINSI YA KUPAMBANA NA MAWAZO MABAYA NDANI YA MOYO WAKO

JIFUNZE JINSI YA KUPAMBANA NA MAWAZO MABAYA NDANI YA MOYO WAKO
                                                      NA; JAMES F. MNZAVA





Bwana Yesu asifiwe sana. Nipende kukukaribisha tena katika somo jingine la jinsi ya kupambana na mawazo mabaya ndani ya moyo wako. Ni somo ambalo nina Imani litabadilisha maisha yako kwa kiasi kikubwa. Biblia inatwambia kwamba awazavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo, je wewe umekua ukiwaza mawazo ya aina gani je wajua mawazo yako ndio wewe mwenyewe? Je wajua ulivyo sasa ni kutokana na mawazo yako uliyokua ukiwaza kabla na sasa? Basi fatana nami katika somo hili na naimani litabadili maisha yako. Karibu sana


NINI MAANA YA MAWAZO        
Ndio kwanza kabisa nipende kuanza kuelezea maana halisi ya mawazo ni nini hasa

MAWAZO ~ Ni fikra na mitazamo zinazotolewa katika akili ya mtu kwa kufikiri mambo yaliyopita, mambo ya sasa na ya badae.

Japokua mawazo hutolewa katika akili ya mtu lakini huhifadhiwa katika moyo wake na ndiko mawazo yanakoishi huko. Akili hutua tu wazo lakini kazi kubwa ipo katika moyo wa mwanadamu katika kuamua na kutekeleza mawazo hayo.

                   MAWAZO YAKO NDIO UHALISIA WAKO

Nia kubwa ya mawazo katika maisha yetu ni kutafuta jibu juu ya yale mambo yanayoonekana magumu kwetu kwa kutumia uwezo wetu wa kimawazo tuliyopewa na Mungu tuweze kuyapatia majibu.




Nikwambie kwamba mawazo yako yanaumuhimu sana katika maisha yako kama utakua namna ya kuuweka moyo wako vizuri ili uweze kuwaza mawazo ya kumpendeza Mungu.
Hebu sasa twende katika maandiko tuangalie jinsi maandiko yanasema nini juu ya mawazo ya mwanadamu.
Mithali 23:7
 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe.

Neno aonavyo katika tafsiri ya (new king james version) NKJV limeandikwa awazavyo moyoni mwake, maneno haya katika biblia yakimaanisha kua jinsi unavyowaza ndani ndani ya moyo wako ndivyo ulivyo.
Mawazo ndiyo yanayakufanya wewe uwe katika ulimwengu huu tunaoishi. Hivyo ulivo sasa ni matokeo tu ya moyo wako umejaza mawazo gani.
Ngoja nikwambie hakuna kitu cha kulinda katika maisha yako vizuri kama moyo ulio ndani yako maana ndio hazina ya mawazo yako, ndilo chimbuko biblia inatwambia haya katika kitabu cha mithali


Mithali 4:23
 Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
Ninaweza kusema kutokana na andiko hili tukiliweka pamoja na lile andiko la Mithali 23 tunapata kitu kikubwa Zaidi cha kujifunza tunaona kwamba jinsi mawazo yako yalivyo ndivyo ulivyo wewe kadhalika na katika kujiona huku ndani yako kuna chemchemi za uzima sasa inategemea unachowaza je ni uzima au ufu.


MAWAZO YAKO YANAWEZA YAKAZAA UZIMA AU UFU
Ndio ngoja nikwambie kama biblia inatwambia kwamba moyo ndani yake ndiko mawazo huwazwa na ndani ya moyo huo huo ndiko chemchemi za uzima zilipo basi ni wazi kua chemchemi hizi zinategemeana sana na kuwaza kwako. Na hatuna budi kuomba kibali kama alichokiomba Daudi mawazo yetu yapate kibali yaani yapate neema ili kuendelea kutunza chemchem za uzima ndani yetu.
Kupitia maandiko haya unaweza kuona mawazo mabaya huharibu maisha yetu na kuharibu uzima uliondani yetu. Na tunachojifunza hapa Zaidi ni kwamba kwa mawazo tu siku zetu zinaweza kufupishwa au kuendela kuongezwa kwa kuendelea kuomba maombi ya kibali kwa kila unachowaza.
Kua makini mpendwa kwa maana kwa kushindwa kulinda mioyo yetu tunamtenda Mungu dhambi mara mbili tukianza katika mioyo yetu pamoja na matendo yetu. Hebu angalia Yesu alipokua akihubiria makutano  na kuwambia kwa kuwaza tu vibaya basi mbele zake unahesabika ushatenda ata kama hujatenda katika mwili wako
Mathayo 5:27-28
 Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;
28  lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

Moyo ndio eneo kubwa la mapambano kati yetu na ibilisi hutuletea mawazo mabaya ili tushindwe kutimiza neno la Mungu katika maisha yetu. Watu wengi hudhani huhesabiwa dhambi kwa matendo yao lakini hawatambua ata kwa mawazo yao kua mabaya ni dhambi kama dhambi nyinginezo na zinahitaji toba ya kweli kabisa mbele za Mungu. Hebu jiulize sasa ni mara ngapi umeomba toba juu ya mawazo yako kua mabaya moyoni mwako je umetamani je umemwazia mwenzako vibaya? Tambua fika kwamba umefanya dhambi na unahitaji toba na msamaha wa Mungu kwako.


VITA VYETU KIROHO HUANZIA KWANZA KWENYE MAWAZO YETU


Ndio hii ndio mbinu kubwa sana ya shetani ya kuwashinda waumini kwa kuwaletea mawazo mabaya katika mioyo yao, kwa kuanza kuwakumbusha mambo ya nyuma na yasioyofaa katika mioyo yao kwa nia ya kuwaharibu Imani zao kwa Mungu ili wasikubalike na Mungu.
Nikwambie kitu kupitia mawazo mabaya yanafanya moyo wako unajisike na kukosa mwelekeo wa kumtafuta Bwana kwa roho na kweli mara zote unakuta mtu anakua vuguvugu tu wa kuanguka na kuinuka kwa sababu ya kushindwa namna ya kuendesha mawazo yake katika njia ya Bwana.




Biblia inatwambia kwamba kabla hatujaingia katika maombi ya kivita ni lazima tuhakikishe tunapambana kwanza na mawazo yasiyotokana na Mungu ili kuweza kupata ushindi katika vita vyetu.

2 wakorintho 10:4

 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;

kumbuka kabisa kabla hujaingia katika maombi yako ya kuomba ahadi za Mungu kwako ni lazima uanze kupambana na mawazo yote yanayojiinua kinyume na kusudi la Mungu katika maisha yako na utauona mkono wa Bwana ukitenda sana katika maisha yako.

Lakini pia mawazo mabaya hutujia kila muda katika maisha yetu jifunze kupambana nayo kiroho hapo hapo ili kutokaa na sumu ya mawazo ya adui itakuharibu jifunze kuomba kiroho na kuomba ndani ya moyo wako katika kuyapinga mawazo haya mabaya.

                       Dhambi huja kwa mawazo

Ndio shetani apohitaji kumuingiza mtu kwenye dhambi yeyote humpa kwanza wazo juu ya dhambi hiyo na mawazo hayo ya kidanganyifu huyaremba ndani ya moyo wake na baada ya kushawishika mtu huanguka katika dhambi angalia (Yakobo 1:13)

Yakobo 1:13-14

 Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.
14  Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.

biblia inatwambia mtu hujaribiwa kwa kuvutwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa kwa kudanganywa, na njia ambayo shetani huitumia kumvuta mtu kuanguka ni kupitia mawazo yake. Angalia sana jinsi uwazavyo na jifunze kuomba maana mawazo ni mlango mojawapo wa dhambi kuingia katika maisha ya mtu.



Na kabla sijaendelea mbele Zaidi mwanadamu kama mwanadamu katika mawazo yake yamegawanyika katika aina kuu  mbili

®Mawazo yenye kibali (mema)
®Mawazo yasio na kibali (mabaya)

Mawazo yenye kibali ni yale yanayompendeza Mungu. Ndio maana daudi anaandika kuhusu ilo katika (zaburi 19:14)
Zaburi 19:14
  Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.

Daudi anasema kwamba mawazo ya moyo wake yapate kibali, yaani yawe mema mbele za Mungu kwa maana alitambua kama ungewaza vibaya katika maisha yake basi angekosa kibali mbele za Mungu.
Nipende kukwambia maana ya maneno haya katika zaburi hii ni kwamba mtu yeyote yule ambaye anawaza mawazo mabaya basi huwa mbali na Mungu na kukosa kibali kwake hatima yake ni kuangamia. Angalia sana mawazo yako maana kwayo ndiyo yatakayokuwezesha kupata kibali kwa Mungu au kukataliwa na Bwana.

MAWAZO MEMA HUKUPA KIBALI MBELE ZA MUNGU

              NB: maana ya kupata kibali ni kupata neema.

Lakini pia aina ya pili ya mawazo ya mwanadamu ni yale ya upotevu yaliteyo adhabu ya Mungu kwa kua ni mabaya. Na maandiko matakatifu yanatwambia katika kitabu cha mwanzo

Mwanzo 6:5-8

Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.
6  Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.
7  Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya.
8  Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.


Biblia inatwambia kwamba pamoja na Mungu kumuumba mwanadamu na kumpa kila kitu katika dunia bado mwanadamu alimuasi Mungu. Na moja kati ya mambo yaliyomchukiza Mungu wakati huo wa Nuhu ni mioyoni mwa wanadamu kulikua na mawazo mabaya na sio siku moja bali ni siku zote za maisha yao walikua wakiwaza mawazo mabaya. Jambo lilimfanya Mungu kujua ata kumuumba mwanadamu. Hebu angalia maneno haya angalia nguvu iliyo ndani yako na jinsi unavyowaza, watu hawa waliwaza mabaya ndipo Mungu akaamua kuwaangamiza kwa gharika.

Lakini katika mstari wa nane biblia inasema kwamba Nuhu alipata kibali machoni pa Bwana yaani likimaanisha Nuhu mawazo yake yalipata kibali kwa kua mema ndipo akaokoka yeye na wanawe.


MAWAZO MABAYA HUMFANYA MUNGU KUGHAHIRI AHADI NA BARAKA ZAKE KWAKO.



Lakini jambo jingine linaloonekana hapa ni Mungu kujuta na kughahiri kwa nini alimuumba mwanadamu kwa sababu ya maovu yake kua mengi pamoja na mawazo yake ambayo ni mabaya kila siku. Mtu wa Mungu hebu angalia hapa kwa makini mawazo tu yalimfanya Mungu kughahiri ata zile Baraka na maisha ya wanadamu kwa kua yalikua mabaya.

Hebu jikagua sasa katika moyo wako je una mawazo mabaya? Au je wewe ni mtu wa kuwaza mabaya moyoni mwako? Tambua ya kwamba unajiondoshea mwenyewe Baraka zako na unamfanya Mungu asikupe kile alichokuahidia hapo mwanzo.


JINSI YA KUSHINDA MAWAZO MABAYA

1.      Weka neno la Mungu la kutosha katika moyo wako
Ndio iyo ndiyo silaha kubwa ya kupambana na mishale ya adui anayoileta katika maisha yetu kupitia mawazo. (Mathayo 4) biblia inatwambia hapa jinsi Yesu aliweza kumshinda shetani kwa neno lililokua moyoni mwake.
Zaburi 119:11
 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
Daudi anasema kwamba moyoni mwake ameliweka neno la mungu ili asimtende Mungu dhambi ndivyo nasi tunatakiwa tulijaze neno la Bwana katika mioyo yetu ili kuziba mianya ya mawazo mabaya katika maisha yetu.

2.     Ishi ukimtegemea Roho Mtakatifu hasa katika kutafuta nguvu zake wakati wa maombi.
Ndio ili uweze kushinda mawazo mabaya ya mwovu ni vyema uweke tegemea lako kwa Roho wa Mungu ili aweze kukuwezesha pindi pale shetani anapojaribu kupambana na wewe kwa njia ya mawazo mabaya ndani ya moyo wako (Mathayo 26:41) ishi ukijua ukitegemea akili zako mwenyewe utashindwa jifunze kuweke tegemeo lako kwake. (Mithali 28:26, Yeremia17:9, Mathayo 26:33)

3.     Jifunze kuulisha moyo wako kwa kumtaka Bwana pamoja na kumwangalia yeye kwa njia ya maombi.
Ndio ili uweze kushinda basi huna budi kulisha moyo wako neno la Bwana pamoja na maombi ili shetani akose nafasi katika maisha yako. Biblia inasema Ayubu aliweza kushinda tamaa zitakazomwangusha katika dhambi kwa kuamua kuweka agano na macho yake ili asivutwe katika mawazo mabaya ambayo yatamwangusha katika dhambi (Ayubu 31:1)

4.     Jitenge na vyanzo vya mawazo mabaya
Ndio watu wengi wamekua wakianguka katika dhambi baada ya wao wenyewe kukubali kuingia wenyewe katika majaribu kwa kuvutwa na tamaa zao wenyewe pasipo kuangalia mazingira wanayoishi kwamba ni hatarishi katika kumwasi Mungu. Jifunze kujitenga na vyanzo vya mazingira ambayo kila siku zinakuzalia mawazo mabaya kwa mfano vipindi vichafu vya television (phonography), picha chafu, maongeze mabaya pamoja na mengine mengi yatokanayo na hayo. Zaidi jikite katika kulitafakari neno la Bwana maana hapo ndipo mafanikio yako yalipo. (Yoshua 1:10)

5.     Tafakari neno la Mungu na epuka uvivu.
Biblia inatwambia kwamba unapolitafakari neno la Bwana ndipo tutakapofanikisha njia zetu. Hivyo ili tuwe wana wa Mungu wenye kibali kwake na mawazo yetu yakubalike kwake ni lazima kuwe na msingi wa neno la Bwana katika maisha yetu ya kila siku. Zipo faida nyingi sana katika kulitafakari neno la Bwana katika maisha yetu. Lakini pia epuka uvivu maana ndioo chanzo kikubwa pia cha shetani kuweka na kupandikiza mawazo mabaya katika mioyo yetu. Hebu angalia jinsi mfalme Daudi alipoanguka katika dhambi ya uzinzi kwa ajili ya kutega kazi na kwenda kuvutwa katika dhambi ya uzinzi.

MUNGU AKUBARIKI KWA KUSOMA.


Imeandaliwa n
a kuandikwa na;                 JAMES F.MZAVA


Mawasiliano;       0762759621, 0653194411, 0625782324


                              jamesmzava@gmail.com 
















                                                                                           

Friday, June 9, 2017

JIFUNZE JINSI YA KUSAMEHE NA KUSAHAU

JIFUNZE JINSI YA KUSAMEHE NA KUSAHAU

                          Na James F. Mzava 

                                    sehemu ya kwanza(1)




Bwana Yesu asifiwe sana. Nipende kukukaribisha tena katika somo jipya la jinsi ya kusamehe na kusahau na nina Imani kua somo hili litakua somo mojawapo la kubadilisha maisha yako kabisa. Ni wazi kua sisi kama binadamu tunapotia katika mambo mbalimbali yapo yanayotufurahisha na yapo yanayotuhuzunisha, na hata mara nyingine tunakua na uchungu mioyoni mwetu kutokana na historia za nyuma ya maisha yetu ambayo tumeyapitia kwa kufanyiwa mambo yasiopendeza katika maisha yetu na kutufanya tushindwe kusamehe na hata tukisamehe bado kumbukumbu zinaendelea kutusumbua sana katika maisha yetu bila kufutika lakini leo nipende kukutia moyo ufatane nami katika somo hili na Mungu atakubariki




NINI MAANA YA MSAMAHA
Ni wazi kabisa katika maisha haya yapo makwazo mengi sana ambayo twapata, mara nyingine hata kwa watu wa karibu nasi wametumika kama mwiba kutuchoma na kutujeruhi mioyo yetu kiasi cha kushindwa kuwasamehe kabisa. Na huenda kwako pia kuna mtu ulishasema “huyu sitamsamehe kamwe” au umewahi kusema “nimemsamehe lakini sitasahau” na mengineyo mengi



Hebu nikwambie kitu hapa je wajua kutosamehe kwako au kutosahau makosa uliyotendewa kunaweza kukakufanya kua chini ya mtu huyo katika moyo wako(kifungo). Basi fuatana nami vizuri utanielewa na kwanza kabisa nianze kuelezea nini maana ya msamaha.


MSAMAHA ~ ni uamuzi wa Mungu au mtu wa kutofuatilia makosa ambayo ametendewa

Au kwa tafsiri nzuri ya neno msamaha kibiblia ni~ kuachilia kosa liende (to let go an offence)

Neno MSAMAHA, kwa maana nyepesi na nzuri limebeba mambo makuu mawili ndani yake;
®        Kutolipiza kisasi japokuwa unayo haki ya kulipiza kisasi.

®       Ni tendo la imani na tena la hiari kwa kuwa unayo sababu, uwezo, na haki ya             kulipiza kisasi kutokana na yale uliyo umizwa.


Nimeona nikupe tafsiri hizo kwanza japo kuna tafsiri nyingine nyingi ila katika somo ningependa kwenda na tafsiri hizo huku tukisimamia neno kuu la msingi wa somo katika Mathayo

Mathayo 6:14-15

  14  Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.
15  Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.




MSAMAHA NI TENDO LA HIARI

Jambo ambalo nataka ujifunze katika mistari hiyo apo juu tambua ya kwamba msamaha nit endo la hiari. Yesu ameweka hiari kwa yeyote yule kuhusiana na msamaha kama twahitaji kusamehewa na Baba ni budi kusamehe ila kama hatuhitaji basi hatutasamehewa vilevile. 





Na kama ni tendo la kihiari lipo ndani ya uwezo wetu kuweza kulibeba au kuliacha.  Na ni kwanini watu wengi wanashindwa kusamehe ni kutokana na kushindwa kujua tendo la kihiari bali wamebaki wakishikilia makosa waliotendewa.na ninaposemea neno hiari simaanishi jambo lingine lolote Zaidi ya maamuzi, namaanisha msamaha ni jambo la kimaamuzi la kuacha kufatilia makosa uliyotendewa na kuanza ukurasa mpya wa furaha



KUSAMEHE KUNAHITAJI GHARAMA YA KUSAHAU MAANA KUTOSAHAU KOSA NI KIDUNGO KWAKO NA SIKU ZOTE MFUNGWA HANA MAAMUZI YAKE MWENYEWE, HIVYO ILE DHAMBI ITAKUTUMIKISHA TU.



Lakini katika hiari hii ni lazima uimbatanishe na Imani. Kwa nini nasema Imani ni kwasababu pindi tunapokosewa mioyo yetu huumia na kujeruhika jambo linalotufanya tushindwe kusamehe na kusahau ata kama ni kwa hiari lakini Biblia inatwambia ya kwamba kazi mojawapo ya Imani ni saburi yaani taraja ambalo latusadia kuganga mioyo yetu iliyoumizwa kutokana na makosa mbalimbali tuliyokosewa



Yakobo 1:2
2  mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.

Ndio unapoingia katika jaribu lolote moja kati ya vitu shetani kutumia kutujaribu ni kwa kutufanya sisi kushindwa kusamehe makosa. Ndio unapoweka Imani juu ya jaribu unalopitia katika kuumizwa kwako na kutendewa uovu chukua hatua ya Imani ambayo ni ya hiari kwa kuachilia makossa hayo ndani ya moyo wako na kukumbuka msahama ambao Yesu alikusamehe makossa yako mengi pale msalabani na wewe achilia kama vile yesu sema imekwisha juu ya maumivu haya na umwachie yeye mwenye Imani yenye saburi kwa ajili ya kukupa tumaini jipya. Na ukifanya ivo utaanza kuona badala ya kuhisi maumivu ya moyo juu ya mabaya uliyotendewa Mungu ataachilia saburi iliyoko ndani ya Imani uliyonayo na kukupa furaha tupu juu ya jambo unalopitia (Yakobo 1:1)



MSAMAHA NI HATUA INAYOANZWA NA MAOMBI

Ndio unaweza ukashangaa lakini ndivyo ilivyo msahama  ni lazima uanzwe katika maombi kwa kuanza kuachilia nafsi yako katika kifungo cha dhambi.

Kama mwanzo nilivotangulia kusema kwamba unaposhindwa kumsamehe mkosaji wako unajiweka katika kifungo cha uovu ambacho kama usipoweza kujua kitakugharimu sana katika maisha yako, hivyo ni vyema wewe kama mkristo kuanza kujifungua katika kifungo cha kutosamehe kwa njia ya maombi.

Pale tu utakapoanza kuwaombea waliokukosea mema na kuanza kuwaombea Baraka za Mungu ziwe kwako ndipo unapojiitoa katika kifungo cha dhambi ya kutosamehe na hapo ndipo utakapoanza kuona hatua kubwa juu ya maisha yako.

 (Mathayo 6:12-13, luka 17:3-4, Marko 11:25)

Endelea kuwaombea mema na mafanikio maana pasipo kujua hilo katika ulimwengu war oho maombi yako hubadilisha ule uchungu wako na kua furaha na kuwapa wakosaji wako uchungu na kukosa Amani. Oooh haleluya!!



MSAHAMA NI JAMBO LA WAZI

Ndio katika msahama kibiblia ni tendo la wazi wala sio la siri kama wengi wanavofanya. Ndio maana Yesu hajatukomboa sisi kwa siri bali aliwambwa msalabani kwa ajili ya kuchukua makossa yetu na akatusamehe kabisa makossa yetu. Na bible inatutaka sisi tufanye ivo ivo


Luka 17:1-4
  Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!
2  Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa.
3  Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe.
4  Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.

Ukiangalia mstari wa tatu kuna neno linasema “mwonye” katika tafsiri nyingine ya biblia linasema “mwambie” usikubali kukaa kimya katika makwazo yanayokuja juu yako maana shetani nia yake ameyaandaa kwaajili ya kukuangusha. Hatua yako ya wewe kumwambia mkosaji wako kinakupa kibali cha kuondokana na anguko la makwazo yanayokujia. Na hii ni siri ambayo watu wengi wameshindwa kuijua badala yake wamekua kimya na kubaki kusema “nimeshamsamehe, siwezi kumsahau yule mtu” na mengineyo mengi, jambo ambalo ni kosa. Tunapaswa sisi kama wana wa Mungu kukiri na kusema kwa wakosaji wetu yale waliotukosea ili msamaha uwepo wa Amani.



Unapoweza kufanya ivo Mungu huleta Amani yake ndani yenu kwa kua Mungu wetu pekee ndiye anayeweza kuufanya mwanzo mmbaya uwe mwema kwa mara nyingine

Wakolosai 3:12
 mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.

Tambua pia unaposamehe ndio mwisho wa kosa acha kuendelea kufikia yaliyopita jifunze kufanya Amani na ata kama yule aliyekukwaza ana jambo jema au amefanikiwa katika jambo Fulani furahi pamoja naye ndio maana ya msamaha ni uwezo wa kuachialia kosa liende na kukaribisha Amani katika moyo wako.



HATUA ZA MSAHAMA

1.      Kubali maumivu na tafuta mlango wa kutokea
Mara nyingine ni inakua vigumu kukubali kuwa umeumizwa na hii ni kutokana na sisi wenyewe kujiaminisha kwamba hatujaumizwa na makosa tuliyotendewa jambo ambalo si sahihi hata kidogo. (1 Wakorintho 10:13)

Tambua ya kwamba hutaweza kutibu maumivu yako pasipo kukubali kwanza kwamba umeumizwa na unahitaji msamaha ili uondokane na maumivu hayo.



 Ndio hii itakusaidia pindi pale unapotaka kusamehe jambo la kwanza ni kukubaliana na kile ulichotendewa.

Andiko hapo juu linasema kwamba Mungu yeye ni mwaminifu na atafanya mlango wa kutokea tambua mtu wa Mungu hakuna lolote litakalokuja kwako ata kama litakua kubwa kiasi gani tambua kabisa Mungu ameshatengeneza mlango ili utoke kwa ushindi. Hebu sasa acha kuwalaumu watu na kuwachukia mtukuze Mungu ata katika watesi wako uuone mkono wa Bwana.


2.     Jifunze nafasi ya Yesu kwako na fanya kama yeye
Ndio pindi unapokua katika hatua ya mfadhaiko hebu anza kutafakari msamaha wa Yesu jinsi alivokusamehe dhambi zako pasipo kujali maovu yako. Nikwambie kitu utakapojikita na ukizama rohoni badaye utaona nguvu za Mungu juu yako za kukutia nguvu na utashangaa kuona u mwepesi na mwenye moyo wa msahama. Ipo nguvu kubwa katika kutafakari kifo na msamaha wa Yesu pale msalabani.



Unapotafakari Zaidi utaona ivi kama Yesu angekataa kutusamehe je tungekua na uzima tena? Hasha!! Tungeangamia wote hakika. Ila yeye katusamehe bila kujali sisi tulivo na huo ndio msamaha wa kweli na wewe tafakari kwanza kama ingelikua ni wewe ndio umekosea na ukagomewa msamaha je ingelikuaje kwako?

Jifunze kwa Bwana na yeye atakuwezesha kusamehe wengine na jifunze kutenda yale unayopenda kufanyiwa kama ulipenda msamaha wa Yesu msalabani basi na wewe samehe ( Mathayo 7:12)




3.      Kumbuka kwamba Mungu alituagiza tusamehane
Mara nyingi katika biblia Yesu alipokua akifundisha juu ya maombi jambo la kwanza kutuambia ni kusamehe kwanza wakosaji waliotukosea ili maombi yetu yajibiwe
Marko 11; 25-26



25  Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.
26  Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]



4.   Achilia maumivu na usahau
Pindi utakapokua umeshatekeleza izo hatua apo juu huna budi tena kuendelea kukaa na maumivu ya makosa yale yale bali achili yote kwa Mungu kwa Imani huku ukisubiri taraja lako ambalo ndio saburi.

Epuka tabia ya kuendelea kufanya mambo yatakayorudisha maumivu yako jitenge na vitu hivo maana kuendelea kua mnyonge na mwenye hasira ndio kutafanya uumie Zaidi achilia mbali maana Amani haiwezi kukaa mahali palipo na uchungu



5.    Endelea kusamehe ata kama kumbukumbu zinarudi
Ndio nipende kukwambia msamaha sio jambo jepesi ndio maana ni gumu sana kutendeka kama ipasavyo wengi wa watumishi wa Mungu hawasamehi na hii ni mojawapo ya dhambi mbaya ambayo itawapeleka watu kuzimu.( 1 Yohana 1:9)



Ndugu jifunze kusamehe najua upo utofauti mkubwa kati ya akili yako na hisia zako, mara nyingi hisia zitaamsha kumbukumbu zako juu ya maumivu uliyoyapata cha kufanya hapo ni kuendelea kuomba rehema na masamaha na Mungu ni mwaminifu atafanya mlango



6.   Jifunze kuombea waliokukosea
Ndio hii itakusaidia sana na hapa unaweza kujiuliza je kama niliokosana nao sina mawasiliano nao tena au hata nikiwasiliana nao kutazuka ugomvi umeshindwa kujua namna ya kuongea na mkosaji wako, usijali hiyo sio kazi yako kazi yako kubwa ni kwenda mbele za Mungu na kuwaombea Amani ya Bwana huko walipo na Mungu atawapatanisha kwa njia yake mwenyewe na kwa uaminifu wake kwenu. (Waefeso 4:31)


Itaendelea…





Imeandaliwa na kuandikwa na;                 JAMES F.MZAVA



Mawasiliano;       0762759621,  0653194411, 0625782324


                              jamesmzava@gmail.com 







AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)

http://bit.ly/3JGDJ4d MWL. JAMES F. MZAVER Minister Truth 0762759621 jamesmzava@gmail.com              AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1) Ukuaji ha...