Tuesday, November 24, 2015

VITA VYA KIROHO (prt 1)

VITA VYA KIROHO (prt 1)

Na:James F.Mnzava



Bwana Yesu asifiwe sana.Nipende kuwakaribisha tena katika somo jingine la vita na mapambano katika ulimwengu wa roho.Wakristo wengi kwa asilimia kubwa na kwa kiwango kikubwa katika kipindi hichi wamekuwa na wakati mgumu pindi wanapoingia katika mapambano katika roho,nah ii ni kutokana na udhaifu katika mapambano.Ungana nami mwanzo hadi mwisho wa somo hili na ni Imani yangu utapanda daraja moja Zaidi.Karibu sana

NINI MAANA YA VITA VYA KIROHO??
Kwanza kabisa nipende kuanza na maneno haya mawili ambayo watu wengi wamekuwa wakishindwa kuyaelewa na kuyatofautisha.Maneno hayo ni maombi ya ukombozi(deliverance) pamoja na maombi ya kiroho.Maombi ya ukombozi yanahusiana na vifungo vya kipepo na kupambana navyo hadi mtu kuwekwa huru.Ambapo maombi ya kiroho ni kupambana,kushinda na
kumweka chini adui anayekaa katika mfumo wa kudanganya,kushtaki na kutujaribu.Inaweza ikawa tafsiri itakayokutatiza sasa ila naimani kadri tunavyoendelea utazidi kuifahamu Zaidi.


Kikawaida vita vya kiroho huja katika maeneo makuu mawili (2)
1.      Eneo la kujilinda
2.    Eneo la kushambulia

Eneo la kushambulia linafanya kazi Zaidi katika kuangusha,kupambana na kuharibu hila,mipango,mashambulizi yote ya adui katika fahamu zetu (2 Wakorintho 10:3).


Ambapo eneo la kujilinda linahusiana Zaidi na kusimama.Baada ya kufanya katika eneo la kushambulia kinachofuata ni kujilinda kwa hila,mikakati na mipango yote ya yule mwovu.

Kuna mambo kama matatu ambayo kikawaida sisi kama wakristo tunaweza tukakumbana nayo pindi tunapoingia katika vita vya kiroho na katika kupambana na shetani.Maana Biblia inatwambia kuwa kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama,bali ni juu ya falme na mamlaka…katika ulimwengu wa roho (Waefeso 6:12).Kwa umakini katika mistari iyo tunakumbana na mambo makuu matatu katika kushindana kwetu.


Waefeso 6:11-18     Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12  Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
13  Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
14  Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
16  zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
17  Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
18  kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

1.UDANGANYIFU,UONGO
Moja kati ya silaha kubwa inayowapiga wakristo wengi na kuwashinda.Na shetani amekuwa akiitumia kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya kudanganya watu na kuwashinda.Ngoja nikwambie uongo ni aina ya roho na pia ni aina ya Imani.Unapomdanganya mtu unamjengea yule uliyemdanganya mazingira ya kuamini uliyomwambia ni kweli.Chanzo kikubwa cha uongo kinaanzia kwenye nafsi na ufahamu wa mtu na ndipo falme na mamlaka zinapofanya kazi Zaidi ili kuweza kuteka watu kwa kiwango kikubwa.


Unaweza ukaombewa na ukawa na Imani kuwa umepona lakini moja ya mbinu ya shetani kukwapua muujiza wako analeta mawazo ya udanganyifu kuwa bado hujapona wewe bado ni mgonjwa na mambo mengine mengi katika ufahamu wako kusudi aondoe Imani ndani yako ushindwe.Ni mbinu kubwa ambayo hutawaliwa na falme na mamlaka kuangusha maombi pamoja na Imani zetu tusiweze kusonga mbele Zaidi.Na kama mkristo ataweza kupambana na kuushinda uongo na undanganyifu wa adui ana nafasi kiasi kikubwa kumshinda adui

Kumbuka hata mwanzo anguko la mwanzo kabisa lilisababishwa na uongo angalia (Mwanzo 3:4)

Usisahau kuwa hizi falme na mamlaka zinafanya kazi zaidi endapo mtu atauhuruhusu uongo uingie katika fahamu zake,na kumbuka kuwa shetani anapoingiza uongo katika fahamu zako anaachilia roho iyo iyo ili na wewe uweze kudanganya wengine.Maana Biblia inatwambia asemaye uongo ni wa ibilisi(baba wa uongo).Chunga sana ili uweze kushinda katika vita vya kiroho epuka uongo maishani mwako.


2.JARIBU,USHAWISHI
Ndiyo,Mara baaya ya shetani kupenyeza maneno na kupanda uongo anaanza kushawishi na kukujaribu kwa hila.Na mara zote uongo na ushawishi wa adui huenda pamoja.(Mwanzo 3:4) Baada ya shetani kumdanganya Eva alianza kumshawishi ``Hakika hamtakufa`` ni neno alilolitumia kumshawishi na kumpamba Eva ili kumpumbaza na kuacha maagizo ya Mungu kwake.Vivyo hivyo hata sisi baada ya adui kuona amepata nafasi katika mioyo yetu kwa njia ya uongo anaingiza ushawishi kupumbaza kabisa maagizo ya Mungu na kukushinda kabisa.Kumbuka kujaribiwa ni kule kuruhusu mwanya wa adui na kuendelea kujipa moyo katika maovu unayotenda maana mara zote shetani ataendelea kukutia moyo usiache kile kibaya anachokuvuta kwacho.


Angalia Mathayo 4 Ambapo shetani alipomjaribu Yesu na kumwambia hata atakapojitupa chini ya mnara hataumia maana malaika wa Bwana wanamlinda asiumie.Vivyo hivyo na shetani anaweza kuleta mitego na vishawishi

Vijana wanaweza kutenda uzinzi lakini bado shetani ndani ya mioyo yao anazidi kuwaambia msijali ni tendo la furaha wala halina madhara ni jambo zuri tu,na wengi wamekua wakianguka na tatizo ni kushindwa na kukwepa kuzijua hila za shetani.

3.MASHTAKA,HUKUMU
Ndiyo kabisa,baada ya shetani kufanya hayo yote anakushitaki maana hadi hapo unakuwa umeshaanguka na huna nguvu tena za kupambana naye.Na kuwa mwangalifu sana maana shetani ni mshtaki wetu

Ufunuo 12:10    10  Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.


Biblia ipo wazi sana kuhusu shetani na inatwambia yeye mchana na usiku ni kutushtaki mbele za Mungu.Wapo wengi san ahata baada ya maombi ya toba bado wanasikia hukumu bado ipo ndani ya mioyo yao si kingine ni mojawapo ya kazi ya adui katika maisha yetu yeye hushitaki hata kwa yale mambo ya nyuma katika maisha yetu,hivyo ni muhimu sana kujua maandiko ya kujisimamia endapo unapoomba maombi ya vita maana adui yeye mara zote hukukumbusha hata kwenye moyo wako kwamba huwezi,wewe ni mwenye dhambi bado,huna nguvu za kunishinda na kadhalika.Ila kama una ufahamu wa neno la Mungu na namna ya kutumia neno kwa ajili ya kupata haki zako itakusaidia sana kumshinda


NAMNA YA KUPAMBANA NA UONGO(deception)
Sawa sawa na andiko katika Waefeso tunazo silaha mbili kwa ajili ya kupambana na uongo wa adui.Tunao mshipi kwa kweli kiunoni (Waefeso 6:14) pamoja na upanga wa roho (Waefeso 6:17).Silaha hizi zote mbili zinalenga kitu kimoja nacho ni kweli.Ila zipo katika sehemu tofauti za vita.
Mshipi wa kweli ni kwa ajili ya kujilinda ambapo upanga wa roho ni kwa ajili ya kushambulia.Hii ikimaanisha kuwa neno la Mungu liko pande zote katika mapambano yetu na adui lipo kwa ajili ya kutulinda pamoja na kutupigania katika maisha yetu


Unatumia mshipi wa kweli kiunoni kwa ajili ya kujilinda na uongo unaoletwa na shetani katika fahamu zetu,ambapo unatumia upanga wa roho kwa ajili ya kukupigania na kushambulia falme na mamlaka ya adui katika maisha yako kupitia ufahamu wako.(Warumi 12:2)

NAMNA YA KUPAMBANA NA USHAWISHI NA JARIBU(temptation)

Yakobo 4:7      Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.


Tambua sio rahisi kumpinga shetani kirahisi maana hutumia kile tunachokifahamu na kukijua katika Kristo (2Wakorintho 10:5-7)
Katika andiko la Yakobo tunaona kuwa zipo njia kuu mbili za kuweza kushinda majaribu,vishawishi vya adui ni kwa kumtii Mungu na kwa kumpinga shetani kikamilifu.Zaidi unavyozidi kumtii Mungu ndivyo Zaidi shetani anazidi kukimbia katika maisha yako.Kumbuka swala hili halihitaji uwe mtu wa maombi ya muda mrefu sana unachotakiwa ni kumtii Mungu Zaidi


UIMARA WAKO KATIKA KUSHINDA MAJARIBU YA ADUI UNATEGEMEANA SANA NA KIWANGO CHAKO CHA UTII MBELE ZA MUNGU


Kumbuka shetani hupambana sana na kiwango cha mtu cha utii na usikivu kwa Mungu na mara zote anaposhinda katika maeneo hayo mkristo yeyote ni lazima atashindwa vita kabisa haijalishi kiwango chake kiroho kipo vipi.


NAMNA YA KUPAMBANA NA MASHTAKA/HUKUMU(Accusation)
Mara zote shetani hupambana nasi hasa katika mambo ya nyuma
tuliyoyatenda kwa kupeleka mashtaka mbele za Mungu.Lakini katika kitabu cha Waefeso 6:16 Biblia inatwambia kuwa ipo ngao ya Imani.Moja kati ya kazi kubwa ya Imani ni kutupa uhakika pindi pale tunapoziungama dhambi zetu kwa Mungu kuwa zimesamehewa na hakuna tena hukumu ndani yetu.(2 Wakorintho 5:17) na dhambi zetu zimesamehewa kabisa (Waebrania 10:17)
Itaendelea…


Imeandaliwa na kuandikwa na;                 JAMES F.MZAVA
Mawasiliano;                                                     0762759621,  0653194411
                              jamesmzava@gmail.com 








No comments:

Post a Comment

AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)

http://bit.ly/3JGDJ4d MWL. JAMES F. MZAVER Minister Truth 0762759621 jamesmzava@gmail.com              AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1) Ukuaji ha...