Tuesday, November 24, 2015

VITA VYA KIROHO (prt 1)

VITA VYA KIROHO (prt 1)

Na:James F.Mnzava



Bwana Yesu asifiwe sana.Nipende kuwakaribisha tena katika somo jingine la vita na mapambano katika ulimwengu wa roho.Wakristo wengi kwa asilimia kubwa na kwa kiwango kikubwa katika kipindi hichi wamekuwa na wakati mgumu pindi wanapoingia katika mapambano katika roho,nah ii ni kutokana na udhaifu katika mapambano.Ungana nami mwanzo hadi mwisho wa somo hili na ni Imani yangu utapanda daraja moja Zaidi.Karibu sana

NINI MAANA YA VITA VYA KIROHO??
Kwanza kabisa nipende kuanza na maneno haya mawili ambayo watu wengi wamekuwa wakishindwa kuyaelewa na kuyatofautisha.Maneno hayo ni maombi ya ukombozi(deliverance) pamoja na maombi ya kiroho.Maombi ya ukombozi yanahusiana na vifungo vya kipepo na kupambana navyo hadi mtu kuwekwa huru.Ambapo maombi ya kiroho ni kupambana,kushinda na
kumweka chini adui anayekaa katika mfumo wa kudanganya,kushtaki na kutujaribu.Inaweza ikawa tafsiri itakayokutatiza sasa ila naimani kadri tunavyoendelea utazidi kuifahamu Zaidi.


Kikawaida vita vya kiroho huja katika maeneo makuu mawili (2)
1.      Eneo la kujilinda
2.    Eneo la kushambulia

Eneo la kushambulia linafanya kazi Zaidi katika kuangusha,kupambana na kuharibu hila,mipango,mashambulizi yote ya adui katika fahamu zetu (2 Wakorintho 10:3).


Ambapo eneo la kujilinda linahusiana Zaidi na kusimama.Baada ya kufanya katika eneo la kushambulia kinachofuata ni kujilinda kwa hila,mikakati na mipango yote ya yule mwovu.

Kuna mambo kama matatu ambayo kikawaida sisi kama wakristo tunaweza tukakumbana nayo pindi tunapoingia katika vita vya kiroho na katika kupambana na shetani.Maana Biblia inatwambia kuwa kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama,bali ni juu ya falme na mamlaka…katika ulimwengu wa roho (Waefeso 6:12).Kwa umakini katika mistari iyo tunakumbana na mambo makuu matatu katika kushindana kwetu.


Waefeso 6:11-18     Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12  Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
13  Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
14  Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
16  zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
17  Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
18  kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

1.UDANGANYIFU,UONGO
Moja kati ya silaha kubwa inayowapiga wakristo wengi na kuwashinda.Na shetani amekuwa akiitumia kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya kudanganya watu na kuwashinda.Ngoja nikwambie uongo ni aina ya roho na pia ni aina ya Imani.Unapomdanganya mtu unamjengea yule uliyemdanganya mazingira ya kuamini uliyomwambia ni kweli.Chanzo kikubwa cha uongo kinaanzia kwenye nafsi na ufahamu wa mtu na ndipo falme na mamlaka zinapofanya kazi Zaidi ili kuweza kuteka watu kwa kiwango kikubwa.


Unaweza ukaombewa na ukawa na Imani kuwa umepona lakini moja ya mbinu ya shetani kukwapua muujiza wako analeta mawazo ya udanganyifu kuwa bado hujapona wewe bado ni mgonjwa na mambo mengine mengi katika ufahamu wako kusudi aondoe Imani ndani yako ushindwe.Ni mbinu kubwa ambayo hutawaliwa na falme na mamlaka kuangusha maombi pamoja na Imani zetu tusiweze kusonga mbele Zaidi.Na kama mkristo ataweza kupambana na kuushinda uongo na undanganyifu wa adui ana nafasi kiasi kikubwa kumshinda adui

Kumbuka hata mwanzo anguko la mwanzo kabisa lilisababishwa na uongo angalia (Mwanzo 3:4)

Usisahau kuwa hizi falme na mamlaka zinafanya kazi zaidi endapo mtu atauhuruhusu uongo uingie katika fahamu zake,na kumbuka kuwa shetani anapoingiza uongo katika fahamu zako anaachilia roho iyo iyo ili na wewe uweze kudanganya wengine.Maana Biblia inatwambia asemaye uongo ni wa ibilisi(baba wa uongo).Chunga sana ili uweze kushinda katika vita vya kiroho epuka uongo maishani mwako.


2.JARIBU,USHAWISHI
Ndiyo,Mara baaya ya shetani kupenyeza maneno na kupanda uongo anaanza kushawishi na kukujaribu kwa hila.Na mara zote uongo na ushawishi wa adui huenda pamoja.(Mwanzo 3:4) Baada ya shetani kumdanganya Eva alianza kumshawishi ``Hakika hamtakufa`` ni neno alilolitumia kumshawishi na kumpamba Eva ili kumpumbaza na kuacha maagizo ya Mungu kwake.Vivyo hivyo hata sisi baada ya adui kuona amepata nafasi katika mioyo yetu kwa njia ya uongo anaingiza ushawishi kupumbaza kabisa maagizo ya Mungu na kukushinda kabisa.Kumbuka kujaribiwa ni kule kuruhusu mwanya wa adui na kuendelea kujipa moyo katika maovu unayotenda maana mara zote shetani ataendelea kukutia moyo usiache kile kibaya anachokuvuta kwacho.


Angalia Mathayo 4 Ambapo shetani alipomjaribu Yesu na kumwambia hata atakapojitupa chini ya mnara hataumia maana malaika wa Bwana wanamlinda asiumie.Vivyo hivyo na shetani anaweza kuleta mitego na vishawishi

Vijana wanaweza kutenda uzinzi lakini bado shetani ndani ya mioyo yao anazidi kuwaambia msijali ni tendo la furaha wala halina madhara ni jambo zuri tu,na wengi wamekua wakianguka na tatizo ni kushindwa na kukwepa kuzijua hila za shetani.

3.MASHTAKA,HUKUMU
Ndiyo kabisa,baada ya shetani kufanya hayo yote anakushitaki maana hadi hapo unakuwa umeshaanguka na huna nguvu tena za kupambana naye.Na kuwa mwangalifu sana maana shetani ni mshtaki wetu

Ufunuo 12:10    10  Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.


Biblia ipo wazi sana kuhusu shetani na inatwambia yeye mchana na usiku ni kutushtaki mbele za Mungu.Wapo wengi san ahata baada ya maombi ya toba bado wanasikia hukumu bado ipo ndani ya mioyo yao si kingine ni mojawapo ya kazi ya adui katika maisha yetu yeye hushitaki hata kwa yale mambo ya nyuma katika maisha yetu,hivyo ni muhimu sana kujua maandiko ya kujisimamia endapo unapoomba maombi ya vita maana adui yeye mara zote hukukumbusha hata kwenye moyo wako kwamba huwezi,wewe ni mwenye dhambi bado,huna nguvu za kunishinda na kadhalika.Ila kama una ufahamu wa neno la Mungu na namna ya kutumia neno kwa ajili ya kupata haki zako itakusaidia sana kumshinda


NAMNA YA KUPAMBANA NA UONGO(deception)
Sawa sawa na andiko katika Waefeso tunazo silaha mbili kwa ajili ya kupambana na uongo wa adui.Tunao mshipi kwa kweli kiunoni (Waefeso 6:14) pamoja na upanga wa roho (Waefeso 6:17).Silaha hizi zote mbili zinalenga kitu kimoja nacho ni kweli.Ila zipo katika sehemu tofauti za vita.
Mshipi wa kweli ni kwa ajili ya kujilinda ambapo upanga wa roho ni kwa ajili ya kushambulia.Hii ikimaanisha kuwa neno la Mungu liko pande zote katika mapambano yetu na adui lipo kwa ajili ya kutulinda pamoja na kutupigania katika maisha yetu


Unatumia mshipi wa kweli kiunoni kwa ajili ya kujilinda na uongo unaoletwa na shetani katika fahamu zetu,ambapo unatumia upanga wa roho kwa ajili ya kukupigania na kushambulia falme na mamlaka ya adui katika maisha yako kupitia ufahamu wako.(Warumi 12:2)

NAMNA YA KUPAMBANA NA USHAWISHI NA JARIBU(temptation)

Yakobo 4:7      Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.


Tambua sio rahisi kumpinga shetani kirahisi maana hutumia kile tunachokifahamu na kukijua katika Kristo (2Wakorintho 10:5-7)
Katika andiko la Yakobo tunaona kuwa zipo njia kuu mbili za kuweza kushinda majaribu,vishawishi vya adui ni kwa kumtii Mungu na kwa kumpinga shetani kikamilifu.Zaidi unavyozidi kumtii Mungu ndivyo Zaidi shetani anazidi kukimbia katika maisha yako.Kumbuka swala hili halihitaji uwe mtu wa maombi ya muda mrefu sana unachotakiwa ni kumtii Mungu Zaidi


UIMARA WAKO KATIKA KUSHINDA MAJARIBU YA ADUI UNATEGEMEANA SANA NA KIWANGO CHAKO CHA UTII MBELE ZA MUNGU


Kumbuka shetani hupambana sana na kiwango cha mtu cha utii na usikivu kwa Mungu na mara zote anaposhinda katika maeneo hayo mkristo yeyote ni lazima atashindwa vita kabisa haijalishi kiwango chake kiroho kipo vipi.


NAMNA YA KUPAMBANA NA MASHTAKA/HUKUMU(Accusation)
Mara zote shetani hupambana nasi hasa katika mambo ya nyuma
tuliyoyatenda kwa kupeleka mashtaka mbele za Mungu.Lakini katika kitabu cha Waefeso 6:16 Biblia inatwambia kuwa ipo ngao ya Imani.Moja kati ya kazi kubwa ya Imani ni kutupa uhakika pindi pale tunapoziungama dhambi zetu kwa Mungu kuwa zimesamehewa na hakuna tena hukumu ndani yetu.(2 Wakorintho 5:17) na dhambi zetu zimesamehewa kabisa (Waebrania 10:17)
Itaendelea…


Imeandaliwa na kuandikwa na;                 JAMES F.MZAVA
Mawasiliano;                                                     0762759621,  0653194411
                              jamesmzava@gmail.com 








Sunday, November 22, 2015

UMUHIMU WA KUHUDHURIA VIPINDI VYOTE KANISANI

UMUHIMU WA KUHUDHURIA VIPINDI VYOTE KANISANI
Na James F.Mnzava




Bwana Yesu asifiwe sana.Nipende kuwakaribisha tena katika somo jingine ambalo Bwana amenipa kibali cha kuweza kushirikiana na wewe la kutambua umuhimu wa kuhudhuria vipindi vyote kanisani.Karibu sana na fatana nami mwanzo hadi mwisho wa somo hili ni Imani yangu somo hili litabadilisha maisha yako.

Kwa muda mrefu sasa kumekua na tatizo hili kubwa karibia kwa makanisa yote duniani hasa kwa wakristo waliookoka kutohudhuria vipindi mbalimbali kanisani wakidhani ni jambo dogo na halina tatizo na ndivyo ilivyozoeleka kwa asilimia kubwa ya waumini wengi duniani.Ila nipende tu kuwaambia kua swala la kuhudhuria vipindi mbalimbali ni swala la kiroho na Mungu mwenyewe aliliagiza hilo kupitia watumishi wake katika maana tofauti ambazo nitazielezea kidogo hapa chini


Kwa kipindi cha miaka ya nyuma Zaidi ya asilimia sabini na kidogo ya waumini walikua na hamu na shauku na kuhudhuria ibada nikimaanisha kati ya watu wanne watatu wao walikuwa na mahudhurio mazuri ya ibada;ila kwa sasa ni chini ya hamsini hadi arobaini ya washirika hupuuzia ibada na kuona ni jambo la kawaida na lisiloweza kuwaletea madhara.
Nipende tu kukwambia Mungu hutujua sana maisha yetu pamoja tunayoyapitia kila siku katika maisha yetu pamoja na mioyo yetu pia.Kila mkristo hasa wale waliookoka inakupasa kuwepo nyumbani mwa Bwana pasipo kujali muda wala nyakati unapokuwa na shughuli nyingi,katika ugonjwa au katika sababu yeyote itakayopelekea kutokuwapo ila unapaswa kuwapo nyumbani mwa Bwana.

Ngoja nikwambie kuwa  mkristo haimaanishi tu kwa yale matendo unayoyafanya siku hadi siku, ila inamaana kubwa Zaidi kushirikiana pamoja na wenzako na kuwa pamoja katika umoja na ndipo Mungu alipoamuru baraka.



TAMBUA KIWANGO CHA BARAKA ZAKO KINATEGEMEANA SANA NA UHUDHURIAJI WAKO KANISANI.MAHUDHURIO DHAIFU HUENDANA PIA NA BARAKA KIDOGO MAISHANI MWAKO


Biblia inatwambia kwamba kwa wale waliookoka ni familia moja katika bwana,na nguvu kubwa ya familia ni kuwa pamoja na kushirikiana vitu kwa umoja.Hivyo tambua kama mkristo fanya bidi sasa kuhudhuria vipindi mbalimbali ili kuweza kukuza kiwango cha baraka zako.


SABABU ZA MSINGI ZA KWANINI TUHUDHURIA VIPINDI KANISANI

·         NI TABIA YA MUNGU~ Waebrania 10:25   Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;
Kama maandiko yanavyotwambia kwamba kama tukifanya dhambi kwa kusudi,basi haitabaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi.Ngoja nikwambie wengi wetu wamekua na sababu nyingi za kutohudhuria kanisani nyingine zikiwa hazina maana yeyote ile ambazo tunaziita ni sababu za makusudi kabisa mbele za Mungu,ni hatari sana maana hakutakua nna dhabihu tena ya dhambi kwa ajili ya watu wanaofanya ivo.Wengi wetu tumezoea kutambua kwa haraka tabia njema kuliko zile nzuri nah ii imetupelekea kufanya tabia mbaya kuliko zile nzuri nah ii ni kutokana na mazoea yetu,na kuwafanya hata wakristo kutohudhuria vipindi kuona ni jambo la kawaida pasipo kujua kua ni tabia mbaya kwa Bwana.Ila tabia ya Mungu ni kukubariki na pia kutuona tunakutana pamoja na kua wamoja kama yeye alivyo Mbinguni

·         NI KILE YESU ALICHOZUNGUMZIA~Luka 14:6  Yesu aliporudi Nazareth mahali alipolelewa Biblia inatwambia alikuwa ni siku ya sabato na aliingia kama ilivyokua ``desturi`` yake.Mahali pengine inaandika kama ilivyokuwa kawaida yake,neno hili desturi likimaanisha alikuwa akifanya jambo hilo mara zote na mara kwa mara siku zake zote.Yesu ndiye kiongozi wetu tunayetakiwa kujifunza kwake na si hivyo tu yeye alifwata kile kilichoandikwa na manabii wa kale,sawa sawa na amri zile kumi za Mungu ``ikumbuke siku ya Bwana na kuitakasa`` yeye pia alifanya vivyo hivyo.Hivyo kama tunavyosema sisi ni wafuasi wa Kristo hatuna budi kushika na kufuata yale yote aliyoyashika na kuyatendea kazi maishani mwetu.


·         NI KUONESHA UPENDO WETU KWAKE.Kwenda kanisani si tu kwa kujengana bali ni tendo la Imani linaloonesha upendo kwa Mungu na kumtii (Mathayo 10:32-33).Ndipo sehemu tukapoweza kumtolea Mungu dhabihu zetu za sifa na shukrani kwake pamoja na matoleo yetu kwa kumshukuru Mungu juu ya yale aliyotutendea katika maisha yetu
Zaburi 22:22 22  Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu.


·         NI MFANO HALISI~Kwenda kanisani ni mfano halisi.Unapojenga tabia ya kuhudhuria kanisani unafanyika kama kielelezo kwa wengine,na pia kama nilivyotangulia kusema hapo mwanzo Mungu pia hukubariki kwa kuwa umeshika amri yake na kuifuata.Kwa wanandoa,wanafamilia endapo mmoja wenu atakua amezingatia kikamilifu kuhudhuria vipindi vyote kanisani tabia hiyo hugeuka na kuwa sumaku ya kuwavuta hata na wale wengine wasiokuwa na tabia iyo.

·         NI MUHIMU KWA USHIRIKA~Wakolosai 3:1616  Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye

 Moja ya sehemu ambapo tunaweza kugangwa mioyo yetu ni kanisani,tunaweza kutiana moyo katika yale magumu tunayopitia kwa kushirikiana pamoja lile ambalo Mungu ameliweka kwetu.Katika maisha tunapitia mambo magumu,masumbufu mengi,matukano,shida,adha na mengine mengi ila tunapokutana pamoja Mungu hutupa neno lake kupitia Roho wake Mtakatifu na kuponya pamoja na kupoza roho zetu.Kuwepo kwa madarasa mbalimbali ya Biblia kanisani pamoja na vipindi mbalimbali kunatengeneza upendo pamoja na kukua kiroho Zaidi.


·         NI MUHIMU KWA KUKUZA IMANI ZETU~Moja kati ya neno zuri sana ambalo huwa napenda kulitumia sana ``Imani haikui yenyewe,bali Imani hukua pamoja na umoja,ufahamu wa Neno la Mungu pamoja na maombi``Ni moja kati ya misemo ninayopenda kuisema mara kwa mara nikimaanisha mahali ambapo mnakutana kwa ajili ya Bwana ni lazima Bwana atazungumza nanyi na moja ya faida ya kusikia sauti ya Mungu ni kuongezeka Imani.Si hivyo tu bali tunaposhirikishana maneno ya Mungu katika vipindi mbalimbali kanisani husaidia pia kukuza Imani zetu siku kwa siku


·         NI MUHIMU KWA KUKUA KIROHO~Huu ni ukweli usiopingika moja kati ya tafiti nilizofanya katika makanisa kadhaa niliyowahi kutembelea waumini wengi ambao hawana tabia ya kuhudhuria vipindi huanguka katika majaribu hasa yale mepesi kabisa.Tatizo hapa ni kutokuwa na elimu ya kutosha katika Mungu,kutohudhuria kanisani kunakufanya ukonde na udhoofu kiroho na shetani anatumia mwanya huohuo kukushambulia kirahisi.

Kupitia ibada tunaweza kumsifu Bwana na kumwabudu na pia kunakusaidia kuweza kupata nguvu pamoja na uwepo wake Zaidi kuliko unapokuwa mwenyewe au katika shughuli zako.


ZINGATIA HAYA YAFUATAYO

Tambua ya kuwa Baraka zako pamoja na mafanikio yako yapo katika vipindi unavyovikosa na kuviruka kanisani.Ndio kama nilivyotangulia kusema mwanzo hatuna budi kama wakristo kuzingatia sana ibada zote kanisani ni sharia ya Bwana wala sio hiari yetu sawasawa na Bwana alivyonena na Musa katika zile amri kumi mlimani.

Tambua Mungu wetu anataka tumwambudu na kumsifu kwa pamoja hekaluni mwake
Yohana 4:23-24 23  Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.
24  Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.


Tamani kiu na matamanio yako yawe ni kuwa pamoja na Mungu,kumwabudu na kumsifu;si tu kwa sababu Mungu hupenda sisi tumsifu bali sisi pia tunahitajika kumsifu yeye kwa hiari na kwa mioyo yetu yote.(Mathayo 22:37-38)

Tambua kila mkristo hana budi kujifunza ili afunze na wengine.(Mathayo 5:6,Waebrania 3:12,1Thessalonike 5:11)

Kwenda kwako kanisani kunakufanya wewe kutembelewa maalumu na Roho mtakatifu.Maana Biblia inatwambia walipo wawili au watatu kwa ajili ya jina langu nitakuwepo katikati yao

Kwenda kanisani kujenga Zaidi mahusiano mazuri na wakristo wengine.Mnapokusanyika sawasawa na mapenzi ya Mungu Amani ya Bwana hukaa juu yetu sote na kutufanya tuwe pamoja na umoja

Kwenda kanisani ni kitendo cha utiifu kwa Mungu.Ndio Biblia inatuagiza kukusanyika na pindi tunapofanya ivyo tunakuwa tumehesabiwa haki mbele zake kwa kuwa watiifu sawasawa na maagizo yake.


Kwenda kanisani kunajumuhisha maombi yetu kwa pamoja.Katika kusanyiko ndio silaha yetu kubwa ya maombi hufanya mambo ya ajabu Zaidi kwa kuunganisha maombi yetu na kuleta matokeo makubwa katika mazingira yetu halisi

Zipo faida na Baraka tele za sisi kuhudhuria ibada nakusihi anza sasa kama ulirudi nyuma hapo awali omba toba kamilifu kwa Bwana na kusudia kuanza upya na Mungu atafanya

KUMBUKA KIPINDI KIMOJA UNACHOKIKOSA NDICHO KIPINDI CHA MAANA ZAIDI CHA KUKUTOA SEHEMU MOJA KWENDA NYINGINE.

AMEN UBARIKIWE!!   BWANA AKUWEZESHE


Imeandaliwa na kuandikwa na;                 JAMES F.MZAVA
Mawasiliano;                                                     0762759621,  0653194411
                              jamesmzava@gmail.com 


Friday, November 20, 2015

TUMIA MAOMBI YA KUFUNGA NA KUOMBA KURAHISISHA MAMBO(2)

TUMIA MAOMBI YA KUFUNGA NA KUOMBA KURAHISISHA MAMBO
Na James F.Mnzava
Sehemu ya Pili(2).



Bwana Yesu asifiwe sana.Nikukaribishe kwa mara nyingine tena katika mwendelezo mwingine juu ya somo tulilolianza la jinsi ya kutumia maombi ya kufunga na kuomba katika kurahishsa mambo.

Nipende pia kukutia moyo kwani kila tatizo unalolipitia lilishapitiwa na wengine kama wewe na wakashida na situ walishinda ila waliacha dawa ili kuwasaidia wengine wanayopitia.Mungu alishafanya njia juu yetu tatizo tunakuwa wazito kushukua hatua.Ni kidokezo kidogo tu nilichoona kitakusaidia;tuendelee Zaidi katika sehemu ya pili ya somo letu.


Kama mkristo uliyeokoka unapaswa kujua ya kuwa mojawapo ya silaha kubwa ya kumshambulia shetani ni maombi ya kufunga na kuomba.

ANDAA MWILI WAKO KABLA YA MFUNGO
Watu wengi wamekuwa wakiumia sana mara baada ya maombi yao ya mfungo kwa sababu ya kutokujua taratibu za kufuata kabla ya kuanza kufunga hasa katika miili yao.Maana unapokua katika maombi ya kufunga bado mwili unaendelea kufanya matendo yake kama kawaida.Hivyo nashauri kwa wale watu ambao wanasumbuliwa Zaidi ya matatizo ya tumbo,nyongo na mengineyo kupata ushauri wa daktari kabla ya kuanza maombi ya mfungo.Ni vyema Zaidi kama ukizingatia haya yafuatayo;

·        Kwa wale wenye matatizo kama nilivyotaja hapo awali ni vyema wakafuata ushauri wa kitabibu Zaidi


·        Weka mipaka katika shughuli zako.Si vizuri unapokua katika maombi ya mfungo nab ado unashughuli nyingi na kazi ni jambo ambalo linaweza kusababisha madhara na kuharibu maombi yako.

·        Fanya mazoezi mepesi.Hii itasaidia kuupa mwili wako hari Zaidi ya mfungo;ni vyema ukawa unatembea kama maili tatu itakusaidia kuondoa na kupunguza kuchoka

·        Tumia maji.Ndio watu wengi mnaweza mkashangaa kwa nini nimeshauri kutumia maji;ukifuatilia maombi kwa undani Zaidi maji yanahusika kwa nafasi kubwa sana maana pindi mwili wako unapoanza kuishiwa nguvu na kuhisi njaa na nyongo inapoanza kutolewa kwa wingi katika utumbo wako vinaweza kukusababishia madhara hivyo ni vyema uwe unatumia maji kidogo pindi unapoingia kwenye maombi nah ii itakusaidia kupunguza makali ya nyogo.


·        Tafuta utulivu.Ndio uhalisia wa maombi ya kufunga yapo katika utulivu epuka kuingiliana na watu na vitu vingine tafuta faragha na utulivu katika maombi yako.

·        Kimbia vishawishi.Ndio watu wengi wamekua wakifunga na bado wanaendelea kujiweka katika maeneo yanayoweza kuharibu maombi yao ya kufunga kwa wao kuendelea kukaa katika sehemu zinazoweza kuwasababishia wao kufungua;kwa mfano kujiweka kati ya watu wanaokula vyakula jambo ambalo ni hatarishi katika maombi yao.

WEKA RATIBA YA KUKUONGOZA
Kwa maendeleo Zaidi ya kiroho pamoja na mafanikio ni vyema uwe na ratiba itakayoweza kukuongoza katika maombi yako;ni kwa kiasi gani utazidi kumtafuta yeye,kulingana yeye,kufunga Zaidi pamoja na kulisoma na kulitafakari neno lake siku hadi siku.

AINA MBALIMBALI ZA KUFUNGA
·        Mfungo wa muda mrefu~wa kutumia maji(unaweza kuchukua siku kadhaa),ila pia kwa walio imara Zaidi wanaweza kufunga kavu bila kutumia maji au matunda.

·        Mfungo wa Daniel~hakuna kutumia chakula,mkate na kitafunwa chochote;ni kutumia maji na juisi pamoja na matunda na mboga mboga.


·        Mfungo wa siku tatu~huu unaweza kuwa mfungo mrefu au mfungo wa Daniel angalau waweza kufunga kwa kutumia mlo mmoja

·        Mfungo mwepesi~Mfungo wa kuanzia asubuhi hadi jioni

·        Mfungo wa Ndoa~Wengi watashangaa sana kuona kua kuna mfungo wa ndoa;ndio upo angalia katika andiko apo chini

1 Wakorintho 7:3-4  3  Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.
4  Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.


Andiko hilo apo lamaanisha mfungo wa ndoa.Biblia inatwambia kua si mke wala mume mwenye amri na mwili wake isipokua mwenzake lakini mstari wa nne ndio wenye lengo kubwa ya kua ikiwa wamepatana kwa muda neno muda hapo linamaanisha mfungo wa muda katika maombi.



Baadhi ya maandiko yahusuyo kufunga;
( 1 Samweli 7:5-6, Ezra 8:21-23, Nehemia 9:1-3, Joel 2:15-16,Yona 3:5-10, Matendo 27:33-37)


Kumbuka Mungu huangalia utayari wako wa moyo katika kufunga kwako wala sio wingi wa siku za mfungo wako katika mfungo.

Kumbuka kumsikiliza Mungu mara kwa mara kwani anaweza akakwambia ufunge kwa siku moja au muda mrefu yote hayo ni yake ila muhimu ni kumsikiliza yeye kwanza.Watu wengi wamekua wakijilazimisha kufunga kwa muda mrefu wakidhani ndio Mungu atawajibu lakini Mungu hilo haliangalii yeye huangalia usikivu pamoja na utayari wako katika kufanya lile alilokuagiza,Haijalishi gharama uliyoitumia ila yeye huangalia Zaidi neno lake kwako.

DONDOO MUHIMU KATIKA MAOMBI YA KUFUNGA NA KUOMBA
Kumbuka kujijengea angalau maombi ya mfungo kwa siku moja au mbili kwa wiki itakusaidia sana na kukuimarisha kiroho

Kumbuka mfungo ni njia mojawapo ya kukutana na Mungu kiurahisi Zaidi na kupata uwepo wake utakaotusaidia kupambana na yule mwovu

Kumbuka kufunga kunatusaidia Zaidi kushinda majaribu ya aina mbalimbali

Mambo magumu na mazito hulainishwa na kuisha kabisa kwa njia ya maombi ya kufunga


Maombi ya kufunga yanakupa upenyo Zaidi ya kuweza kufikia Baraka zako kirahisi

Kumbuka maombi ya kufunga yanakuwekea ulinzi Zaidi na maadui zako wote

Kupitia maombi ya kufunga Mungu hushugulika na mahitaji yetu mengine ambayo hata hatujamuomba kutokana na unyenyekevu wetu kwake

Kupitia maombi ya kufunga ngome na mamlaka ya adui huangushwa chini na kushindwa kabisa

Maombi ya kufunga yanaongeza kibali Zaidi cha kusikilizwa na Mungu


Kupitia maombi ya kufunga Mungu hugeuza mabaya yote na kuwa mema.

ZIPO FAIDA NYINGI MNO KATIKA KUFUNGA NA KUOMBA.ANZA SASA NA UTAUONA MKONO WA MUNGU KWENYE MAISHA YAKO!!

Amen!! UBARIKIWE

Imeandaliwa na kuandikwa na;                 JAMES F.MZAVA
Mawasiliano;                                                     0762759621,  0653194411
                              jamesmzava@gmail.com







Thursday, November 19, 2015

TUMIA MAOMBI YA KUFUNGA NA KUOMBA KURAHISISHA MAMBO

TUMIA MAOMBI YA KUFUNGA NA KUOMBA KURAHISISHA MAMBO
Na James F.Mnzava
Sehemu ya kwanza(1)



Bwana Yesu asifiwe sana.Niwakaribishe tena katika somo jingine tena ambalo Bwana amenipa kibali tushirikishane maneno yake katika somo jingine la maombi ya kufunga na kuomba kwa jinsi yanavyofanya magumu kuwa mepesi.Fatana pamoja nami sasa.

NINI MAOMBI YA KUFUNGA NA KUOMBA??
Watu wengi makanisani wamekuwa wakifanya maombi ya kufunga na kuomba katika namna tofauti tofauti ambazo nyingine zimekuwa zikileta faida na pia nyingine zimekuwa zikiwaletea madhara katika maisha yao pasipo kupata majibu katika maombi yao.


Nakumbuka kuna dada mmoja alikua anasumbuliwa sana na tatizo la kupata kupata mtoto kwa muda mrefu bila ya kupata bila kupata mafanikio.Hivyo akaamua kwenda katika huduma mojawapo ya maombezi na baada ya kuombewa kwa muda mrefu bado tatizo lilibaki pale pale ila mwendesha maombi alimwagiza yule dada achukue maombi ya kufunga na kujifungia ndani kwa muda wa siku saba bila kula wala kunywa;na kweli yule dada kwa kuwa aliteseka na tatizo hilo aliamua kufanya ivo lakini siku moja kabla ya kumaliza maombi yake alishindwa na kufariki.Je wewe unajifunza nini hapo? Je ni Bwana ndio aliwaagiza wale wanamaombi kumwambia yule dada kufunga hadi kufa au ni wao wenyewe?.Hapo nadhani jibu sahihi unalo.

Tafsiri halisi ya neno kufunga ni kuweka kando yale mambo yote yaliyo na maana,au unayoyapendelea kwa ajili ya kumtafuta Bwana.

Unapofunga kunakuruhusu kuuadibisha mwili wako kwa ajili ya matamanio yako ya kiroho kwa Mungu wako.

Hapo nadokeza kwamba yeyeote yule anapokuwa katika mfungo anautumikisha mwili wake na kuuadibisha kwa ajili ya kukua,kuongezeka kiroho Zaidi;ndio maana hapa haijalishi umeokoka au la kila mtu anaweza kufanya ivi kwa ajili ya Imani yake mwenyewe.Mapepo yanafunga,waabudu sanamu wanafunga pia,wachawi na washirikina na wasioamini wanafunga pia,hii ni kutokana na kuongeza matamanio yao katika roho zao juu yay ale wanaoyoyaamini.Vivyo hivyo ata sisi tulioamini Kristo tunafunga kwa ajili ya kuongeza matamanio ya roho zetu kwa Bwana na kufiisha matendo yale ya mwili na kuongeza tunu Zaidi katika roho zetu.


Unapofunga unajiongezea udhabiti na uimara katika maisha yako ya kila siku
Kumbuka neno kufunga linalomaanisha kuuadibisha mwili wako kwa ajili ya matamanio yako ya kiroho kwa Bwana kunafaa Zaidi na kua na maana Zaidi endapo ule muda uliouzoesha mwili wako kwa ajili ya mambo yako mengine uutumie muda huo kwa ajili ya kumtafuta Bwana kwani kufunga pasipo kuomba na kuutafuta uso wa bwana ni kazi bure.

Jinsi maandalizi ya kujiandaa kwa maombi yako ndio kutakakuamua mafanikio katika maombi yako.Namaanisha maandalizi mabovu kutapelekea kuwa na matokeo mabovu hivyohivyo.Kumbuka kufanya maandalizi katika roho,nafsi na mwili wako pia ili uweze kupata matokeo mazuri ya kufunga kwako.Hebu tuangalie kidogo hatua muhimu za mwanzo katika kufunga.

HATUA MUHIMU ZA MWANZO KATIKA KUFUNGA.

·        WEKA NIA NA MALENGO Kwa nini unafunga? Ni kwaajili ya kupokea tunu na kupandishwa madaraja kiroho,kwa ajili ya usikivu Zaidi kiroho,mwongozo Zaidi,uponyaji Zaidi,kwa ajili ya matatizo magumu yaliyoshindikana,kwa ajili ya neema maalumu ya kutuwezesha kuhimili majaribu tunayokutana nayo.Unapofahamu haya yatakusaidia sana ili uweze kujua umuhimu Zaidi katika maombi yako;na pia kukufanya uombe kwa Imani Zaidi pamoja na malengo.


Kupitia maombi ya kufunga tunajinyenyekesha kwa Mungu ili kumruhusu Roho Mtakatifu aweze kuchochea roho zetu Zaidi,kuamsha makanisa pamoja na kuponya nchi yetu(2Nyakati 7:14)

·        KUMBUKA KUWEKA AHADI NA KUDHAMIRIA   Omba kwa ajili ya aina ya maombi utakayoenda kuomba wakati unapofunga.Yesu aliwaagiza wanafunzi wake kwamba wanapaswa kuomba na kufunga ili mambo mengine kwenye maisha yao yaweze kwenda (Mathayo 6:16 , 9:14-15).Kabla ya kufunga ni lazima mtu awe ameweka ahadi au mipango ifuatayo ili aweze kutoba Zaidi katika ulimwengu wa roho mambo hayo ni kama;

1)     Ni muda gani utafunga? Hili ni swali la muhimu sana kujiuliza kama umeamua kuingiza kwenye maombi ya kufunga na kuomba utafunga kwa siku moja,tatu,saba,wiki au mwezi mzima(ila kwa wale ambao bado hawajawahi kuomba maombi ya kufunga na kuomba ni vizuri kwao kuanza kidogo kidogo)

2)   Ni aina ipi ambayo Mungu amekuagiza kufunga.Ni jambo jema kumsikiliza Mungu sana juu ya kile anachokwambia je utakua unatumia maji au kinywaji chochote hapo ni kutokana na maagizo maalumu kutoka kwa Mungu

3)   Ni aina gani ya shughuli itaicha kwa muda.Katika kufunga ni jambo la kiroho na la faragha Zaidi ambalo unahitaji Zaidi kuwa karibu sana na Mungu hivyo kwa wale watu wenye shughuli nyingi ni vyema kuzipunguza au kuzisitisha kwa muda kwa ajili ya Bwana

4)   Ni muda kiasi gani utakao utumia kwa ajili ya kuomba na kusoma neno.Kufunga kunaendana sana na kuomba pamoja na kusoma neno la Mungu kwaiyo ni vyema sana kupangilia muda wa kutosha juu ya ilo.



Kupitia mambo hayo manne ni mambo ya msingi sana ya kuzingatia pindi unapoaamua kuingia kwenye maombi ya kufunga na kuomba.

·        ANDAA ROHO YAKO.    Kumbuka msingi mkuu wa maombi yetu ni toba kwanza ni vyema kuanza kwa kuandaa roho zetu kwaajili ya kumruhusu Mungu kusikia maombi yetu.Hakikisha unatubu dhambi kwanza na kuwasamehe waliokukosea kwanza.Pia zingatia haya unapoandaa roho yako

1)     Omba ili Mungu akukumbushe pale ulipoanguka na makossa uliyomkosea


2)   Kiri na ungama kila dhambi ambayo Roho Mtakatifu anayokukumbusha kuitubia;na pokea msahama wa Mungu kwako(1 Yohana 1:9)

3)   Wasamehe wale wote waliokukosea omba msamaha kwa wale wote uliowakosea (Mathayo 11:25 ,Luka 11:4)

4)   Kuwa msikivu na mwelekevu sawasawa na Roho Mtakatifu anavyokuelekeza.


5)    Muombe Mungu akujaze na Roho Mtakatifu kama alivotuahidi (Waefeso 5:18,1 Yohana 5:14-15)

6)   Tafakari juu ya ukuu wa Mungu katika maisha yako ya kila siku;tafakari neema yake,huruma zake pamoja na mambo yote aliyokutendea

7)    Anza maombi yako ya kufunga kwa kwenda kwa moyo wa kutarajia kupokea

Itaendelea….

Imeandaliwa na kuandikwa na;                 JAMES F.MZAVA
Mawasiliano;                                                     0762759621,  0653194411
                              jamesmzava@gmail.com 








AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1)

http://bit.ly/3JGDJ4d MWL. JAMES F. MZAVER Minister Truth 0762759621 jamesmzava@gmail.com              AKILI ILIYOFANYWA UPYA. (1) Ukuaji ha...